LIVE STREAM ADS

Header Ads

WATU WENYE ULEMAVU WILAYANI NYAMAGANA WASHINDWA KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI KUTOKANA NA GHARAMA ZA UCHAGUZI.

Katibu wa Chama hicho Omari Matajago Sendama (Kulia) akizungumza na GB Pazzo @Metro Fm & Binagi Media Group (Kushoto).
Na:George GB Pazzo
Chama cha Watu wenye Ulemavu CHAWATA Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza, Kimesema kuwa Watu wenye ulemavu wameshindwa kujitokeza kwa ajili ya kuwania kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kutokana na kushindwa kumudu gharama za uchaguzi ndani ya yama vya Siasa.

Katibu wa Chama hicho Omari Matajago Sendama aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Radio Metro, juu ya ushiriki wa watu wenye ulemavu katika kuwania nafasi za uongozi na namna watu hao walivyoshiriki katika zoezi la uandikishaji wa wapiga kura lililomalizika hivi karibuni Mkoani Mwanza.

Sendama alisema kuwa katika zoezi la Uandikishaji Wilayani Nyamagana, hakukuwa na malalamiko yoyote kutoka kwa watu wenye ulemavu kwa kuwa watu hao walikuwa wakipewa kipaumbele zaidi hali iliyopelekea mwamko wao katika kujiandikisha kuwa mkubwa.

Kuhusiana na ushiriki wa watu wenye ulemavu katika kuwania nafasi za uongozi Wilayani Nyamagana, Sendama alibainisha kuwa ofisi yake haijapokea jina lolote la mtu mwenye ulemavu ambae amejitokeza kwa ajili ya kuwania nafasi ya kugombea uongozi wowote ule kutokana na kushindwa kumudu gharama za uchaguzi zinazotozwa na vyama vya siasa hapa nchini.

Alisema kuwa awali baadhi ya walemavu walikuwa wakijitokeza kwa ajili ya kuwania kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, lakini jitihada zao zilikuwa zikishindikana kutokana na kushindwa kulipia gharama za kampeni ambazo mgombea hutakiwa kuzilipa ambapo ameongeza kuwa watu wenye ulemavu wanaomba utaratibu huo kubadilika na badala yake wapewe fursa ya kugombea bila kuwepo kwa gharama zozote.

Kwa pamoja Christina Mnana Mwiye ambae ni Mjumbe wa CHAWATA Mkoa wa Mwanza pamoja na Rehema Idd ambae ni Mratibu wa Kikundi cha akinamama wenye Ulemavu Wilaya ya Nyamagana cha Disability Dream Pilot Project walisema kuwa mbali na watu wenye ulemavu kushindwa kumudu gharama za uchaguzi, pia wanakabiriwa na changamoto nyingi ambazo ni pamoja na kukosa kuaminiwa na wapiga kura kwa minajiri kuwa hawawezi kuwa viongozi.

Walisema kuwa bado wanakabiliwa na ukosefu wa mazingira bora ya kupata elimu hali ambayo inawafanya kukosa fursa za kuwania nyazfa za uongozi ambapo wamehimiza kuwa viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi wa mwaka huu wanapaswa kuhakikisha kuwa wanawasemea wanapata haki zao za msingi ambazo ni pamoja na kupata elimu na kushirikishwa katika uteuzi wa nafasi mbalimbali za uongozi.

Hata hivyo licha ya CHAWATA Wilaya ya Nyamagana kubainisha kuwa hakuna mlemavu yeyote aliejitokeza kugombea katika uchaguzi wa Mwaka huu, Radio Metro Fm imebaini kwamba yupo mmoja ambae amejitosa kuwania kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi CCM ili kugombea ubunge Jimbo la Nyamagana.
Katibu wa Chama hicho Omari Matajago Sendama (Kulia) akizungumza na GB Pazzo @Metro Fm & Binagi Media Group (Kushoto).
Christina Mnana Mwiye ambae ni Mjumbe wa CHAWATA Mkoa wa Mwanza
Rehema Idd ambae ni Mratibu wa Kikundi cha akinamama wenye Ulemavu Wilaya ya Nyamagana cha Disability Dream Pilot Project.

No comments:

Powered by Blogger.