MWANZA WATAKIWA KUCHANGIA MAHITAJI YA POLISI JAMII ILI KUIMARISHA ULINZI NA USALAMA.
Wa kwanza Kulia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara ndogondogo katika Masoko na Minada kwa Wilaya za Nyamagana na Ilemela Justine Sagara akifuatiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishina Msaidizi wa Polisi Charles Mkumbo pamoja na Viongozi wa Jeshi la Polisi hilo katika kilele cha mafunzo ya polisi jamii kwa wanachama wa jumuiya hiyo kilichofanyika jana katika Uwanja wa Magomeni Kirumba Wilayani Ilemela.
Na:George GB Pazzo
Wananchi
Mkoani Mwanza Wametakiwa Kushirikiana kwa ukamilifu na Vikundi mbalimbali vya
Ulinzi shirikishi, ili kuhakikisha kuwa Wanadumisha amani na Usalama katika
maeneo yao.
Rai hiyo ilitolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Mwanza Kamishina Msaidizi wa Polisi Charles Mkumbo, wakati akifunga mafunzo
ya Polisi Jamii yaliyotolewa kwa Wanachama wa Jumuiya wa Wafanyabiashara
ndogondogo katika Masoko na Minada kwa Wilaya za Nyamagana na Ilemela.
Kamanda Mkumbo alisema kuwa wananchi wanao
wajibu wa kuendelea kudumisha amani, ulinzi na Usalama uliopo hapa nchini ikiwa
ni pamoja na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazovikabili vikundi vya
polisi jamii.
“Kwa mapungufu mbalimbali kama mlivyosema kuwa
mnakabiriwa na ukosefu wa sare, filimbi na sare nawasihi wananchi wasisite
kuhamasishana ili kuchangia kwa mfumo wa harambee ili kuyatatua mapungufu hayo
badala ya kutegemea serikali au jeshi la polisi pekee”. Alisema Kamanda Mkumbo.
Kwa Upande wake Mkufunzi wa Mafunzo hayo Sajenti
wa Polisi Mkoani Mwanza Clement Kabatila alisema kuwa wahitimu wa mafunzo hayo
wamefundishwa Uzalendo, Ukakamavu, nidhamu pamoja na utii ambavyo vitawasaidia
katika kupambana na uhalifu katika jamii.
Nae Mwenyekiti wa Umoja huo Justin Sagara
aliwataka wanachama waliohitimu mafunzo hayo kutimiza majukumu yao kwa
utii na usawa na kwamba atakaebainika kukiuka
maadili ya kazi yake Umoja huo utamchukulia hatua kali za kinidhamu.
“Nawaomba mkafanye kazi kwa utii, mkatende haki
na kuheshimu sheria bila kumuonea machinga. Na naomba niwaambie kwamba askari
yeyote ambae hatakuwa mtii hatafanya kazi minadani kwani tutamuondoa kufanya
kazi na sisi”. Alisisitiza Sagara.
Jumla ya Wanachama 34 wanawake wakiwa ni wawili
kati ya 50 kutoka Jumuiya hiyo ya Wafanyabiashara ndogondogo katika Masoko na
Minada kwa Wilaya za Nyamagana na Ilemela ambao walianza mafunzo ya Polisi
jamii mwezi wa pili mwaka huu wamehitimu mafunzo hayo, ambapo katika risala yao
wameomba kusaidiwa vitendea kazi ikiwemo pingu, filimbi, tochi pamoja na sare
kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao ya biashara pamoja
na majumbani.
TAZAMA PICHA HAPA
TAZAMA PICHA HAPA
No comments: