LIVE STREAM ADS

Header Ads

SEHEMU YA KWANZA: UGONJWA WA KISUKARI UNAVYOATHIRI JAMII.

Inline image 2
Picha kwa msaada wa mtandao jinsi ugonjwa wa kisukari unavyoathiri sehemu za mwili
Judith Ferdinand
Kuna magonjwa mengi yanayosumbua  binadamu kwa sasa ulimwenguni kote,huku wataalamu mbalimbali wakijaribu kutafuta tiba bila mafanikio,jambo ambalo magonjwa hayo yanaendelea kutesa na kusababisha vifo vya watu mbalimbali kila kukicha.

Miongoni mwa magonjwa hayo  ni ugonjwa wa kisukari, kwa sasa unashika kasi katika kushambulia binadamu ulimwenguni, kuacha watu wakiwa walemavu na kuwa tegemezi na kuacha pengo katika familia,jambo linalopelekea ongezeko la watoto yatima  na kupoteza nguvu kazi ya taifa.

Ugonjwa wa kisukari umezoeleka katika jamii kuwa ni  wa kurithi kutoka kwa mababu na mabibi, asilimia kubwa unawapata watu ambao umri wao umesogea(wazee kuanzia miaka 50 na kuendelea),ila kwa sasa imekuwa tofauti maana  hadi watoto wa umri kuanzia  miaka 6 anaweza kuugua ugonjwa huo.

Wengi wanasema kuwa ugonjwa huu wakisukari kwa sasa unasababishwa na msongo wa mawazo, kutofanya mazoezi kwani hasa watu wa mjini hawapendi kutembea kwa umbali mrefu na badala yake atapanda gari,pikipiki na usafiri mwingine hata kama sehemu anayoenda ni karibu, pia ulaji wa vyakula hovyo ambavyo siyo vya asili bali vile vilivyotengenezwa kiwandani.

Agnes Lucas mmoja wa wana familia ambayo ilimpoteza mtu muhimu katika familia kutokana na ugonjwa wa kisukari, anaelezea namna ugonjwa huo unavyotesa na jinsi ulivyosababisha akampoteza shangazi yake kipenzi.

Anaanza kwa kusema "kweli nauchukia ugonjwa wa kisukari na sipendi hata kuuusikia kwani umesababisha shangazi yangu kipenzi kututoka ikizingatiwa kuwa alikua ni kiuongo muhimu katika familia,tazama alivyokufa kwa mateso,kukonda ,hii inatokana na kutopatiwa elimu juu ya ugonjwa huu.

Agnes anasema kama wangepatiwa elimu juu ya kujikinga kabla ya kuugua na baada ya kuugua ugonjwa huo,hakika ingesaidia,waathirika wa ugonjwa huo kuishi maisha marefu.

Anaeleza namna ukosefu wa elimu kuhusu ugonjwa huo unavyoweza kupelekea waathirika wa kisukari kuaga dunia/kufariki mapema.

Ilikuwa mwaka 2012 marehemu shangazi alipogundulika na ugonjwa huo, hii ni baada ya kuwa anahisi kiu mara kwa mara,huku koo likikauka,mwili kuishiwa nguvu,kuhisi njaa muda wote na kuwa mtu mwenye hasira,baada ya kupimwa katika hospitali ya Mkoa  Wa Mwanza Sekour Toure ndipo alishauriwa kuanza kliniki lakini kwa bahati mbaya hawakumpa maelekezo ya namna anavyotakiwa kula chakula.

Kwani mtu ambaye ameisha athirika na ugonjwa huu,anatakiwa kula milo sita kwa siku,pia kwa kiasi kidogo huku akizingatia makundi  matano ya chakula na kuzidisha mbogamboga, kufanya mazoezi,kupima mara kwa mara,na kutumia dawa kwa usahihi, jambo ambalo watu wengi hawalifahamu.

Hata hivyo anaiomba serikali na wadau mbalimbali kuwapatia elimu wananchi,namna ya kuweza kujikinga na ugonjwa huu, lakini pia kuwatunza walioathirika na ugonjwa huo na jamii inatakiwa kuwa nao karibu wagonjwa hao na kuaacha kuwanyanyapaa hata kama watakua ni wakali ambapo kwa kufanya hivyo itawasaidia kuishi kwa muda mrefu.

Naye Muuguzi wa hospitali ya Rufaa Bugando Mkoani Mwanza Kitengo cha Ugonjwa wa Kisukari (Diabetic Unit) Leah Mhana anaelezea juu ya ugonjwa huo.

"Ugonjwa wa  Kisukari ni  hali  ambayo utokea wakati sukari  inapokuwa nyingi kupita kiasi katika damu kwa sababu  ya upungufu au ukosefu wa kichocheo kiitwacho  insulin". Anafafanua Mhana.
Mhana anabainisha kuwa ugonjwa wa kisukari umegawanyika katika makundi mawili ambayo ni;
Kundi la kwanza ni wale ambao kongosho lao linatoa  kichocheo kiitwacho Insulin lakini haitoshelezi matakwa ya mwili.

Mgonjwa ambaye yupo katika kundi hilo anaweza kutumia tiba bila dawa,kama kufanya mazoezi kwa ajili ya kupunguza uzito, kupunguza kula vyakula vya wanga na mafuta,endapo tiba hii haitaweza kurekebisha kiwango cha sukari mwili,wataanzishiwa vidonge, kama navyo vitashindwa atalazimika kutumia sindano ya Insulin.
Itaendelea, Imeandaliwa na Judith Ferdinand; 0757804962 Kwa msaada wa mtandao na mashirika ya habari.

No comments:

Powered by Blogger.