LIVE STREAM ADS

Header Ads

SEHEMU YA KWANZA YA MAKALA IITWAYO "NIA".

Huwezi kufanikiwa kwenye jambo lolote mpaka utakapokuwa na NIA, Nakumbuka kuna mtu mmoja alisema maarifa ni nguvu (knowledge is power), hii ni nusu ya ukweli , kwani maarifa yanakuwa na nguvu pale tu yanapowekwa kwenye vitendo na mtu ili aweze kutimiza jambo fulani, wewe hata uwe umesoma una degree 20 kama ukishindwa kuweka katika vitendo kile ulichokisoma bado elimu yako haijakusaidia na haina manufaa kwako na jamii yako.
NIA, ni hisia kali ambayo mtu anakuwa nayo kuhusiana na suala fulani ambalo analipenda. Mtu mwenye NIA huwa anaushawishi mkubwa na hufanikiwa kwa kiasi kikubwa kwenye kila jambo analofanya.
Nakuhakikishia kuwa hata tajiri huwa hamsaidii masikini kama masikini asipowasha NIA yake kwa tajiri maana tajiri nae huwa anaangalia NIA, je ni kweli huyu mtu anahitaji huu msaada na anafanya juhudi zote kuupata? Baada ya kujiridhisha katika haya ndipo humsaidia mtu huyo.
NIA ni moja ya kitu ambacho kina nguvu ya ajabu na mtu anaweza kutumia NIA kuweka katika vitendo elimu aliyojifunza juu ya kitu fulani, uzoefu wake katika kutenda mambo fulani, na maarifa aliyokuwa nayo. Sijui namna nyingine ya kufanya kitu chochote pasipo kuwasha NIA juu ya jambo unalotaka kulifanya.
Maneno ya kuongea ongea tu yasiyo na NIA huwa yanakuwa hayana nguvu na wakati mwingine yanaweza kuboa na kukera watu. Hivyo ni muhimu kujifunza namna kuwasha na kuzima nia yako na wakati mwingine unaweza ukawasha NIA sehemu ambayo haihitajiki na watu wakakuona wewe ni mwehu, kwa mfano mtu anakwenda kuhubiri sokoni au kazini sasa sisemi kuhubiri kwa NIA ni vibaya ila sehemu hizi sio sahihi.
Kama umeshawahi kuchunguza vizuri mtu ambaye hana NIA huwa pia ana tabia ya kupinga vitu na kuwa kinyume na watu hata kama hakuna sababu ya msingi ya kuwa kinyume, na hii pia ni moja ya tabia mbaya ambayo huwa inaharibu utu wa mtu.
Nakumbuka kipindi nasoma Chuo Kikuu Cha DODOMA kuna Mwalimu alikuwa anaweza akafundisha kwa zaidi ya masaa mawili, lakini kila nilipokuwa naulizwa mwalimu kafundisha nini baada ya somo, ambacho nilikuwa nakumbuka ni kwamba alifanikiwa kuteka uwepo wangu darasani.
KWA NINI NIA INAKUWA NA NGUVU KIASI HICHO?
Ni lazima uelewe kwamba ubongo wako na ubongo wa mwenzio unapokea na kutuma taarifa za mitetemeko ya fikra mbalimbali, ni kama kituo cha redio, ubongo huwa unapokea na kutuma taarifa kwa mtu mmoja hadi mwingine pasipo hata mtu kuongea na njia hii inajulikana kama telepath kwa kiingereza.
Wakati umewasha NIA, unatengeneza mtikisiko ambao unaweza kutoka na kuenda kugusa watu wengine haraka na utafikia wale watu ambao umenuwia iwafikie hata kama watakuwa hawaongei na hiki ni kitu ambacho kinajulikana na Wanasaikolojia kwa muda mrefu.
Wauzaji wazuri(good sales men ) ambao wanafanya vizuri ni wale wanaowasha NIA yao kwa wateja kabla hata hawajaanza kuelezea kile wanachokiuza na huwa wanafanikiwa kwa kiasi kikubwa. Ukienda kumuuzia mtu kitu chochote hakikisha unawasha NIA yako kwanza ndipo unamuuzia kinyume na hapo hatanunua hicho unachotaka kumuuzia.
Kama ulivyoona katika maelezo haya NIA ina tabia ya kuambukiza, na pia unaona kwamba huwa inatumiwa na wale wanaoijua na huwa wanafanikiwa katika kila wanalolifanya.
Nataka nikwambie hata huo mpango ulionao kama ukienda kumwelezea mtu pasipokuwa na usipokuwa na NIA huyo unaemuelezea hataweza kupata mtetemeko wa mpango wako kwa hiyo hata kama ni kukusaidia hatoweza maana hujawasha NIA, jifunze namna ya kuwasha NIA yako katika kila kitu unachokifanya.
Andrew Carnegie ambae ni tajiri mkubwa aliyewahi kuishi miaka ya nyuma aliwahi kusema hivi "Kama ukimwajiri mtu mmoja mwenye NIA katika kiwanda chako ambacho una maelfu ya wafanyakazi, huyu mtu mwenye NIA atawashawishi hao maelfu ya watu wengine katika jambo ambalo anataka kulifanya haijalishi hilo jambo ni la kubomoa au ni la kujenga. Lakini pia alisema ili aweze kumpandisha mtu cheo kazini kigezo cha kwanza alichokuwa anaangalia kilikuwa ni NIA (ule uwezo wa mtu kujielezea mwenyewe kwa NIA yenye mhemko).
Pia aliwahi kusema kwamba NIA ni sifa kubwa katika uongozi nawe pia utakuwa shahidi kuwa hata viongozi wanaopendwa na watu wengi ni wale wenye NIA ya ajabu ambao wanaonekana katika maongezi yao na wanaotaka kweli katika kubadilisha maisha ya watu.
Namkumbuka kiongozi wangu mmoja alikuwa Waziri wa Mikopo kipindi nasoma Chuo Kikuu, alikuwa na NIA ya ajabu na alikuwa anaongea kwa hisia kali sana alikuwa tayari kufanya jambo lolote lile ili wanachuo wapate (hela ya kujikimu) kwa wakati na pindi fedha ilipochelewa alikuwa wa kwanza katika kudai haki na kama ni mgomo wa Amani yeye alikuwa anakaa mbele kabisa. Sitashangaa siku nikisikia kawa kiongozi mkubwa Tanzania maana ni moja ya watu niliowahi kukutana nao wenye NIA ya ajabu.
Kitu ambacho watu hawajui ni kwamba wanasheria wengi waliofanikiwa sio wale ambao wanajua mambo mengi sana yanayohusiana na sheria ila ni wale ambao wanajua namna ya kushawishi mahakama pamoja na jopo zima la majaji kwa kuamini kwao katika kesi zao na ambao wana uwezo mkubwa wa kujielezea wenyewe kwa NIA thabiti.
Itaendelea tena...
Tufuatilie instagram LIFESECRETSCOMPANY ujifunze zaidi.

No comments:

Powered by Blogger.