LIVE STREAM ADS

Header Ads

SEHEMU YA TATU YA MAKALA IITWAYO "NIA".

Soma HAPA Sehemu Ya Kwanza Ili Twende Sawa.
NIA INA UMUHIMU GANI NA NIFANYE NINI ILI KUIBUA NIA ILIYO NDANI YANGU?
NIA inasababisha vitu mbalimbali kufanyika katika jamii yetu. Kuna mwalimu mmoja aliwahi kusema kwamba NIA ni kama switch unayoiwasha na kuizima ambapo ikiwashwa huleta mabadiliko katika jamii na ikizimwa vitu havibadiliki. NIA pia husababisha vitu kufanyika katika ubora wa hali ya juu pasipo kulipua kwa sababu mtu hufanya kitu kutokea moyoni na hunuia kuona mabadiliko katika kile anachokifanya.
NIA huvutia watu, kati ya vitu vinavyovutia kwa mtu, NIA inaweza ikawa ni miongoni mwa tatu bora, ni kitu ambacho kinamfanya mtu kuvutia katika maisha yake binafsi, kazi yake anayoifanya na katika mahusiano yake na watu mbalimbali. 
Wanasiasa na wanamuziki wanaopendwa ni wale walio na NIA katika kufanya siasa na miziki yao. Hivi umeshawahi kuangalia Diamond anavyoimba na kucheza kwa hisia? NIA ndio inamfanya yeye kufanya vile na unaona namna anavyopata tuzo mbalimbali za kitaifa na kimataifa.
NIA ni njia pekee yenye nguvu ya ajabu katika mawasiliano, mtu mwenye NIA huongea sio na mdomo tu bali na mwili pia(body language) na hata ukimsikiliza sauti yake huwa unasikia tofauti na mtu asie na NIA, NIA hufanya maneno na ujumbe kuwa na nguvu kwa sababu huwa yanaongewa kwa hisia na hisia hizo huonekana katika sauti pamoja na lugha ya mwili(body language) ambapo hali hii hufikisha ujumbe kwa nguvu ya ajabu katika mkusanyiko wa watu.
NIA pia hufanya maisha kuwa ya furaha, mtu asie na NIA huwa hana furaha katika maisha, mtu anaelala tu hana kitu cha kumsukuma kesho asubuhi kuamka akakifanye huwa hana furaha, maisha ni mazuri hakuna sababu ya kuwa na huzuni, tafuta kinachokupa furaha kisha kitendee kazi na uwashe NIA yako, NIA ni kama jua linalowaka ndani ya miili yetu ambalo linatuangazia katika maisha na kufanya maisha kuwa marahisi, yaliyo na mwanga na ya kufurahia.
VITU GANI MTU ANAWEZA KUFANYA ILI KUWASHA NIA YAKE.
Katika kila hali mbaya ambayo unapitia jaribu kutafuta uzuri uliopo ndani yake, saa zingine huwa tunapatwa na matatizo mengi sana katika maisha lakini watu wengi hawajui kwamba ndani ya yale matatizo huwa kuna mbegu iliyojificha. Kama ukiweza kuichunguza na kuiona basi utakuwa umefanikiwa, watu waliofanikiwa huwa wanatafuta jambo zuri katika kila baya wanalokutana nalo na nakuhakikishia hata upitie jambo baya kiasi gani kama ukiamua kukaa chini ukatafuta kitu kizuri katika hilo baya ulilonalo utakiona tu na ukisha kiona basi NIA yako juu ya hiko kitu huwaka. 
Napolion Hill aliwahi kusema in every adversity there is a seed of equal benefit, yaani katika kila baya kuna mbegu ya faida, ni jukumu lako wewe na mie kutafuta hiyo mbegu ya uzuri kisha uifanyie kazi.
Tafuta jambo ambalo unapenda kulifanya (your calling) na hii ndio sababu kubwa kuliko zote ya kumfanya mtu kuweza kuwasha NIA, watu wengi wanafanya kazi ambazo hawazipendi wapo tu ili wapate mshahara. 
Hali hii imewafanya kudumaa akili,kutokuwa wabunifu, kuomba Mungu wiki-end ifike maana hawapendi kwenda kazini n.k. Kitendo cha kufanya kitu ambacho hukipendi huuwa NIA ambayo ipo ndani yako na hivyo hutoweza kufanya kazi kwa umakini. 
Katika maisha yako fanya kile unachokipenda tu na kumbuka tupo hapa duniani kwa muda mfupi hivyo hakuna haja ya kufanya mambo ambayo hayapo ndani ya moyo wako. Mwalimu wangu anayeitwa John Maxwell aliwahi kusema hivi "uamuzi upo mara mbili, moja kuchagua unachotaka kufanya kisha unaanza kukifanya, mbili kuchagua ambacho hutaki kufanya kisha haufanyi. Hivyo basi fanya tu kile ulichochagua kufanya ili uwashe NIA iliyopo ndani yako.
Tafuta namna ya kubadili vitu, kama kuna jambo lolote ambalo wewe hulipendi katika jamii yako na unaona kabisa unao uwezo wa kuligeuza na kulifanya kuwa bora basi ni vema ukalichukulia hatua mara moja. 
Huenda labda ni huduma fulani unaona haitolewi sawa, au ni uongozi haupo vizuri, chukua jukumu la kugeuza hali hiyo na hiyo itawasha NIA iliyopo ndani yako na utafanya jambo hilo vizuri, lakini pia upande wa pili wa pont hii ni kwamba kama unafanya kitu ambacho hukipendi basi badili na tafuta kile unachokipenda.
Juzi nilikuwa naangalia mahojiano ya Depark Chopra na wanafunzi wa chuo fulani nchini India, kuna mwanafunzi akawa analalamika na kusema kwamba anachukia magazeti ya India kwa sababu yanaandika habari zisizoelimisha jamii hata kidogo. 
Nilipenda Chopra alivyomjibu ambapo alimwambia kuwa anatakiwa asomee uandishi wa habari ili abadili hiyo hali na ayafanye hayo magazeti yaelimishe namna anavyotaka yaelimishe na hali hii iliwasha NIA kwa yule dada.
Jaribu kuwauliza wateja wako kuhusiana na namna unavyowahudumia, watu majasiri huwa wapo tayari kupokea ukweli hata kama unauma. Usiogope kuuliza kisa unaogopa kuambiwa unafanya vibaya kwa sababu watakapo kuambia kwamba bado huduma yako siyo nzuri ndipo hapo wewe utajituma zaidi na hii itachochea NIA iliyoko ndani yako ili kuhakikisha unatoa huduma nzuri na ya kuvutia kwa wateja wako.
Elewa kiundani, jifunze zaidi juu ya kile unachokifanya, huwezi kufanya vizuri biashara ya mtandao, au kuelezea kiundani namna kitu fulani kinavyofanya kazi kama hukifahamu. NIA inawaka pale unapojua kiundani juu ya kitu unachokifanya hivyo basi usifanye kitu ambacho hukielewi kiundani, tenga muda wa kutosha jifunze kiundani mpaka ukielewe kisha toka nenda ukakifanye ndipo NIA yako itawaka maana unajiamini na unajua kwamba unajua juu ya hiko kitu.
Tafuta watu wa kuwaiga (models) ambao unawaona wana NIA, jaribu kuwafuatilia ni vitu gani huwa wanafanya(rituals) kabla ya kuja kwenye umma kisha nawe fanya kama wanavyofanya, kama ni waalimu au wahamasishaji basi nunua dvd na cd zao kisha sikiliza mara kwa mara, usiwe na ubahili wakati unataka kujifunza kitu ambacho unajua kitabadilisha maisha yako. Mimi binafsi nina watu wangu maalumu ambao huwa nawafuatilia na kuwasikiliza mara kwa mara ili kuibua NIA ndani yangu akiwemo Tony Robbins, Napolion Hill, Clemenstone na Pastor Norman Vincent Peale.
Fanya jambo moja kwa wakati, usitake kukamilisha mipango yako yote kwa wakati mmoja watu wengi wanajaribu kutaka kufanikisha mambo mengi kwa wakati mmoja mwishowe hujikuta wanafanya chini ya kiwango yaani wanapata average. 
Chagua jambo moja unalotaka kulifanya na lishughulikie kwa asilimia 100 mpaka ulitimize na hii itazidi kuchochea NIA iliyo ndani yako na baada ya kumaliza jambo moja fanya jambo jingine tena.
Itaendelea...
IMEANDALIWA NA LIFE SECRETS COMPANY.

No comments:

Powered by Blogger.