LIVE STREAM ADS

Header Ads

SHILINGI BILIONI 230 ZAPOTEA NCHINI KUTOKANA NA AJALI ZA BARABARANI.

Na:Judith Ferdinand
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza Baraka Konisaga amesema kuwa takribani shilingi billion 230 nchini zimepotea kutokana na ajali za barabarani huku ajali hizo pia zikigharimu maisha ya watu pamoja na mali zao.

Pia alisema kuwa ajali nyingi hutokea katika makutano ya reli na kugharimu maisha ya watu na hivyo kuitaka Mamlaka ya Usafirishaji Majini na Nchi Kavu SUMATRA kutoa elimu kwa  madereva na wananchi ili kuepukana na ajali hizo.

Akizungumza katika semina ya ajali za barabarani iliyofanyika jana Jijini Mwanza na kuwakutanisha wadau wa usafirishaji wakiwemo madereva na Sumatra, Konisaga alisema kuwa vyanzo vikuu vya ajali nyingi nchini ni mwendo kasi, uchakavu wa magurudumu na wizi wa alama za barabarani unaofanywa na watu wachache.

“Tumekuwa tukishirikiana na veta kusaidiana nao ili kupunguza ajali za barabarani lakini bado zinatokea, ni vyema Sumatra wakaanza kutoa elimu pia hata kwa watu wanaotumia barabara kwa njia ya kawaida ili tuondoe tatizo la ajali.” Alisema Konisaga.

Alisema kuwa, makosa ya kibinadamu yamekuwa ya kiongoza katika ajali za barabarani na hivyo kuitaka Sumatra kuhakikisha kabla dereva hajapewa gari lazima awe na leseni na kufanyiwa ukaguzi.

Naye Meneja usalama barabarani na mazingira SUMATRA kutoka Makao Makuu Geoffrey Silanda alisema kuwa baada ya kuona ajali nyingi zimekuwa zikitokea katika makutano ya reli wameamua kutoa semina elekezi kwa madereva mkoani Mwanza.

Alisema kuwa katika kutoa semina hizo wametoa elimu kwa madereva katika mikoa  ya Tanga, Tabora, kigoma na Mwanza na kwamba semina hizo zitaendelea katika mikoa mingine.

No comments:

Powered by Blogger.