LIVE STREAM ADS

Header Ads

UMOJA WA WANUNUZI WA PAMBA WILAYANI KAHAMA HATARINI KUFIRISIKA.

Na:Shaban Njia
Umoja wa Wanunuzi wa zao la Pamba katika Wilaya Kahama Mkoani Shinyanga UMWAPA huwenda usifikie lengo la kupata faida katika kufanya biashara hiyo kwa mwaka 2015/2016 kutokana na kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika ununuzi wa zao hilo ambalo limeonekana kulimwa kwa kiwango chini Mkoani Shinyanga.

Mwenyekiti wa Umoja huo Mhoja Ndegesela anasema kuwa kwa msimu huu Umoja huo uliwekeza jumla ya Shilingi Bilioni 3.5 katika kipindi cha mwaka 2015/16 lakini hadi sasa ambapo msimu huo unatarajia kumalizika UMWAPA imepata takribani shilingi Milioni 800 tu.

Ndegesela alisema kuwa pamoja na kutoa mafunzo kwa maafisa Ugani wao ili waweze kushirikiana na wale wa Serikali lakini bado imekuwa ni vigumu kwa wakulima wa zao la pamba kuongeza kiwango cha mavuno ya zao hilo ambalo kwa sasa linaonekana kutolimwa kwa wingi.

“Sisi kama umoja wa Wanunuzi wa zao la Pamba baada ya kuona maafisa Ugani wa Serikali ni wachache katika maeneo yanayolimwa Zao la Pamba, tuliamua kuwafundisha maafisa ugani wetu ili kusadia na wale wa Serikali kwa gharama zetu ili wakulima waweze kulima Kilimo chenye tija lakini bado mambo hayajaenda vizuri kwa Mwaka huu”. Alisema Ndegesela.

Pia Mwenyekiti huyo wa UMWAPA alisema kuwa kitendo cha kuchafuliwa  Pamba ikiwa ni pamoja na kuweka maji katika zao hilo hakusababishwi na Wakulima bali kunatokana na Mawakala wanaosimamia ununuzi wa zao hilo katika maeneo yao.

Alisema kuwa baadhi ya Mawakala wamekuwa wakiweka maji na michanga katika Pamba ili kuweza kuongeza uzito katika mizani huku fedha nyingine za ununuzi wakizitumia katika mambo yao binafsi hali ambayo imekuwa ikiwatia hasara makampuni yanayotoa fedha hizo kwa ajili ya ununuzi.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo hakusita kuiomba Serikali iangalie jinsi ya kumsadia Mkulima wa zao la Pamba ikiwa ni pamoja na kuweka Kilimo cha Umwagiliaji maji kwa zao hilo kama ilivyo kwa zao la Mpunga kwani hali ya hewa imekuwa ni tatizo kubwa kwa wakulima kwa kutokuwa na mvua za kutosha.

“Serikali ikitusaidia kwa kuweka kilimo cha Umwagiliaji katika zao la Pamba kama ilivyo kwa wenzetu wanaoilima mpunga badi kunaweza kumsaidia mkulima kuwa na moyo wa kulima Pamba na kuongeza uzalishaji kuliko ilivyo kwa sasa mvua hakuna na wakulima wanaonyesha kukata tamaa ya kulima zao hilo”. Aliongeza Mhoja Ndegesela.

No comments:

Powered by Blogger.