LIVE STREAM ADS

Header Ads

WANAWAKE WAFANYABIASHARA NA WAJASIRIAMALI MKOANI MWANZA WAPIGWA MSASA KUJIKOMBOA KIUCHUMI.

Judith Ferdinand
Zaidi ya Wanawake 100 ambao ni Wafanyabiashara na Wajasiriamali Mkoani Mwanza wamepatiwa mafunzo juu ya namna ya kukuboresha ushiriki wao katika shughuli  za kimaendeleo ikiwemo mikakati ya kupambana na umasikini.

Akizungumza jana Jijini Mwanza katika uzinduzi wa kongamano la kwanza kwa Wanawake Wajasiriamali na wafanyabiashara katika Masokoni nchini, Mkurugezi wa bodi ya watendaji wa shirika la Equality for Growth (EFG) Emmanuel Tuju alisema kuwa lengo la kongamano hilo ni kumwezesha mwanamke kutumia zaidi mali, nguvu na jitahada ili kujiletea maendeleo na kulinda haki yake katika umiliki wa mali.

“Sisi kama Shirika la Equality For Growth tumeamua kuleta elimu hii nchi nzima kwa kuanzia mikoa saba ambayo ni Mwanza, Tanga, Shinyanga, Lindi, Mtwara, Mbeya na Dar es salaam ili  kuhakikisha kuwa mfanyabiashara mwanamke anapata haki ya kumili mali zake”.

Mkurungezi mtendaji wa EFG Jane Magigita alisema wanawake wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokuwepo na sheria inayosimamia haki zao  kutokana na  mapungufu makubwa yaliyopo, utashi thabiti wa viongozi serikalini pamoja na sera kutumika kisiasa zaidi ya maendeleo.

Alisema ili kuinua maendeleo ya sekta hii, viongozi wanapaswa  kutunga sheria  na kuzisimamia kwa ajili ya kuboresha miundombinu pamoja na kutoa fursa pamoja na haki sawa kwa wananchi walio katika sekta hiyo.

Aidha baadhi ya washiriki wa kongamano hilo ambao pia ni wafanyabiashara wa sokoni walisema, wanakumbana na changamoto mbalimbali zikiwemo za utozwaji wa ushuru sawa na wafanyabiasha wakubwa.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wafanyabiashara katika Soko la Mkuyuni Jijini Mwanza Veneranda Joseph  alisema kuwa Halmashauri hiyo imeshindwa kutofautisha wafanyabiashara wadogo na wakubwa wakati wa kuwatoza ushuru kwani wote  wanalipa kiwango sawa.

Naye Mwenyekiti wa Soko Kuu Mkoani Mwanza Ahmed Nchola alisema, ni vema halmashauri ikatenga   eneo husika kwa wafanyabiashara wanaopanga bidhaa zao chini, kwani wengi wao hawaliipi kodi kama wanavyolipa wa maduka na meza.

Hata hivyo biashara ndogondogo huzalisha ajira kwa watu million 2.4 kwa mwaka huku watu 440,000 huingia katika sekta isiyo rasmi  hawa hujumuisha wahitimu wa darasa la saba, waliopunguzwa kazi, wastaafu na wahitimu kutoka vyuoni.

No comments:

Powered by Blogger.