LIVE STREAM ADS

Header Ads

WAZEE WILAYANI MAGU WAIOMBA SERIKALI KUWAIMARISHIA ULINZI.

Na:Judith Ferdinad
SERIKALI imeombwa kuimarisha ulinzi kwa wazee pamoja na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale watakaobainika kujihusika na vitendo vya mauaji ya wazee nchini.

Wito huo ulitolewa jana na wazee wa kijiji cha Lumeji, kata ya Sukuma, iliyopo wilayani Magu mkoani Mwanza, walipokuwa wakiongea na Wanahabari.

Akiongea  kwa niaba ya wazee hao, Tabu Busumabu alisema, kutokana na kuendelea kwa mauaji ya wazee katika maeneo mbalimbali nchini, serikali iwaimarishie ulinzi na kuwachukulia hatua za kisheria watakaoonekana kuhusika na mauaji hayo.

"Tunaiomba serikali na jeshi la polisi ituimarishie ulinzi hasa kipindi hiki tunapoelekea  kwenye uchaguzi mkuu, matukio mengi ya mauaji kwa wazee mara nyingi hutokea kipindi kama hiki, na sisi tukiuwawa vijana wetu hawatakuwa na maendeleo," alisema Busumabu.

Naye Yurita John wa kata ya Nyigogo iliyopo wilayani hapo, ambaye ni mtoto wa mama aliyewahi  kukatwa mapanga na watu wanaodaiwa kuwa ni ndugu zake  baada ya wazazi wake kufariki dunia, kwa madai kuwa yeye ndiye aliyehusika na vifo vyao, alisema baada ya mama yake kufanyiwa kitendo hicho maisha yao yamekuwa ya shida kutokana  na kuwa tegemezi katika familia hiyo.

Hata hivyo Muhamasishaji wa jamii wa shirika la Maperece lililopo wilayani humo, linaloshughulika na utetezi wa haki za wazee linalodhaminiwa na shirika la Help Age International, Levitas  John alisema, mauaji hayo baada ya kuonekana yakitokea kwa wazee, hata watu wa rika tofauti na hao yametokea yakihusishwa na tuhuma za kishirikina.

Aliongeza kuwa , kutokana na wazee wengi kuonekana wakiishi katika mazingira magumu, shirika hilo limefanikiwa kutetea masuala ya afya kwa wazee ambapo kupitia wao, hospitali ya wilaya hiyo imeweza kutenga kitengo maalumu kwa ajili ya matibabu kwa wazee.

Aidha kwa niaba ya wazee waliokuwa wakipata matibabu katika hospitali hiyo, Charles Misungwi,  alilishukuru shirika hilo kwa kuweza kutetea haki zao na kufanikisha wao kupata matibabu bila malipo.

Vilevile Mratibu wa Mradi wa Afya bora kwa Wazee wa Shirika hilo, Grace Julius alisema, ili kuwainua kiuchumi na kuacha kuwa tegemezi wameweza kuwafundisha wazee masuala ya ujasiriamali kwa kutengeneza dawa za asili sambamba na utumiaji wa vyakula vya asili  ambavyo vitawasaidia kupunguza magonjwa.

No comments:

Powered by Blogger.