KUELEKEA UCHAGUZI MKUU, MWENYEKITI UVCCM WILAYA YA ILEMELA ATOA NASAHA ZAKE KWA WANANCHI.
Kulia ni Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza Herry James
Judith Ferdinand
Wananchi Mkoani Mwanza wameshauriwa kutogombana na kutoleana lugha ya matusi, sababu ya vyama vya siasa hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu , kwani vyote vinapita na nchi itabaki, ili kulinda tunu ya amani tulionayo.
Wito huo ulitolewa juzi na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), wilaya ya Ilemela Herry James katika mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea udiwani kata ya Nyamanoro, ulifanyika katika uwanja wa ghana katani hapo.
James alisema, unapogombana kwa ajili ya viongozi wa kisiasa, inasababisha muhusika kupata ulemavu, kufungwa na kupoteza maisha, huku wanasiasa wanaendelea kula raha bila ya kuwakumbuka wanyonge.
Pia alisema, wanasiasa wengi ni waigizaji na hawana uadui wa kudumu zaidi ya siasa, lakini katika maisha ya kawaida ni marafiki na wanashirikiana katika mambo mbalimbali, na kuwaacha wananchi wasiyo jua maana yake wanapata matatizo.
"Ngoja niwaambie ndugu zangu, siasa hazina uadui wa kudumu, kwani viongozi wengi katika maisha ya kawaida wanashirikiana sana, mfano, kuna kiongozi mmoja kwa miaka 8, alituhumiwa na kuchafuliwa na chama kimoja cha siasa nchini, lakini sasa wanakaa meza moja na kula pamoja huku wananchi mkibaki na alama za mshangao,” alisema James.
Hata hivyo aliwaomba, wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ifikapo oktoba 25, bila ya kufanya vurugu kwani matokeo yote watakua nayo mawakala wa vyama vyao, ili kujiepusha kupata ulemavu, kufungwa na kupoteza maisha kwa ajili ya wanasiasa ambao hawawezi kuwakumbuka.
Naye Katibu Siasa na Uenezi kata ya Kirumba Wessa Juma aliwaomba wananchi hususani vijana kutokubali kutumika kama chambo kisiasa, kwani watu wengi wamepoteza maisha, wamebaki na ulemavu sambamba na kufungwa huku familia zikibaki maskini na wahusika wakiendelea kuishi salama.
"Kuna matukio tofauti yanayohusika na vurugu za kisiasa yalitokea hapo nyuma nchini, huku vijana wengi walitumika baadhi yao wakipoteza maisha, kuwa walemavu na wengine wapo magerezani wakipata tabu, ingawa wanasiasa waliokuwa wanawatetea hawawajali,” alisema Juma.
No comments: