MWASELE HERBALIST YASHAURI JAMII KUTUMIA ZAIDI VYAKULA VYA ASILI.
Mganga Mkuu wa Kituo cha Tiba Asilia (Mwasele Herbalist Clinic) Dk.Saguda Masanja akimpima presha mmoja wa Wanahabari Wetu.
Picha na Judith Ferdinand.
Judith Ferdinand na Getruda Ntakije
Jamii imeshauriwa kula vyakula vya asili na kuachana na vile vinavyosindikwa viwandani, ili kuepuka magonjwa mbalimbali.
Wito huo ulitolewa juzi na Mganga Mkuu wa kituo cha tiba asilia cha Mwasele ( Mwasele Herbalist Clinic), Saguda Masanja, wakati akizungumza na Majira kwenye maonyesho ya 10 ya biashara ya Afrika Mashariki, yanayofanyika katika uwanja wa chuo cha Dar es Salaam Institute of Technology (D.I.T), tawi la Mwanza.
Dk. Masanja alisema kuwa jamii kwa sasa inasumbuliwa na maradhi mbalimbali ikiwemo kisukari, presha,madonda ya tumbo na mengine, kutokana na ulaji wa vyakula ambavyo siyo vya asili.
“Jamii kubwa hasa ya mjini ndio waathirika wa magonjwa kama kisukari, hii ni kutokana na kula vyakula ambavyo siyo vya asili na havina tija katika mwili zaidi ya kushibisha tumbo”. Alisema Dk. Masanja.
Pia alisema kuwa jamii imejisahau na kuacha kufanya mazoezi jambo linalosababisha mwili kushindwa kufanya kazi ipasavyo na kuwa rahisi kushambuliwa na magonjwa.
Aliongeza kuwa magonjwa hayo yanatibika endapo mgonjwa atakuwa muaminifu kwa kufuata mashariti na ushauri alioelekezwa na mtaalamu wa afya.
Hata hivyo aliiomba jamii kujijengea tabia ya kupima afya mara kwa mara ili kuweza kutambua na kugundua tatizo mapema.
No comments: