LIVE STREAM ADS

Header Ads

WAUMINI WATAKIWA KUWAEPUKA VIONGOZI WA DINI WANAOHUBIRI SIASA KATIKA NYUMBA ZA IBADA.

Na:Neema Emmanuel
Waumini wa dini nchini wametakiwa kuwaepuka viongozi wa dini ambao wamesahau majukumu yao ya kuhubiri neno la Mungu na badala yake wamekuwa wakijikita katika itikadi za kisiasa.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Watoa Uzima wa Kimataifa kutoka Shirika la Life Givers International Godfrey Fungo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza.

Alisema ili kudumisha amani na utilivu wa nchini, waumini wa dini mbalimbali wanatakiwa kuwa makini na viongozi wa kiroho ambao wameingilia majukumu  ya wanasiasa ambayo hayawahusu.

“Nawaomba waumini watafakari na kufanya uamuzi sahihi wa kuwapigia kura viongozi wanaowataka bila kufuata mkumbo au kushawishiwa na viongozi wa madhehebu wa dini zao wakati wa kupiga kura”. Alisema Fungo.

Aidha aliwataka viongozi wote wa dini kuomba kwa ajili ya amani na kuwashauri watu wapige kura kwa busara zao bila  kuonyesha waziwazi msimamo wa kuegemea upande fulani wa vyama vya kisiasa kwa kutambua kuwa wao ni viongozi wa kiroho ambao hawajali itikadi za kisiasa.

Pia Fungo alisema kuwa endapo mtumishi wa Mungu  anataka kuwa mwanasiasa basi ajipambanue ili  ijulikane  wazi kuwa yeye ni mwanasiasa, asijaribu kuchanganya vitu vyote viwili ambavyo vinaweza kuleta uvunjifu wa amani.

Hata hivyo aliwataka wagombea wote katika nafasi mbalimbali za uongozi wachunge ndimi zao wakati wa kujinadi katika kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea kote nchini na kwamba wajiadhari kutamka maneno yasiyo na vitisho bali waongee mambo ya maendeleo.

No comments:

Powered by Blogger.