LIVE STREAM ADS

Header Ads

MWENYEKITI BARAZA LA WAZEE CHADEMA KATA YA SABASABA TARIME AUAWA NA WATU WASIOJULIKANA.

Mwili wa aliekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema Kata ya Sabasaba, Tarime ukiagwa kwa ajili ya kwenda kupumzishwa.
"Kila Nafsi itaonja Mauti, hakuna atakaekiepuka kikombe hicho. Sie tu mavumbi na tutarudi mavumbini.
Hakuna aijuae siku, saa, dakika wala sekunde za yeye kurudi Mavumbini kama vitabu vitakatifu vinavyotuambia. Ni Mwenyezi Mungu pekee anaejua kuja kwetu na kuondoka kwetu duniani. Binadamu hana Mamlaka ya kukatisha maisha ya binadamu mwenzake tofauti na Mungu tu.
Tangu kuanza kwa kampeni katika majimbo ya Tarime kumekuwa na matukio ya kinyama kabisa hasa ya kukatisha maisha ya binadamu wenzetu, wazee kwa vijana ambao taifa linawategemea kwa maendeleo ya nchi yetu.
Ni siku chache baada ya kuripotiwa mauaji ya ndugu zetu jimbo la Tarime mjini upande wa Chadema kwa kuuawa wakati wakitoka kwenye Kampeni.
Juzi Team Matiko tumeshirikiana na ndugu zetu wa kata ya Sabasaba kumsindikiza mzee wetu aliekua Mwenyekiti wa Baraza za Wazee Chadema kata ya Sabasaba Mzee Mwita Bokombe kwenye nyumba yake ya Milele baada ya kuuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana.
Mitazamo ya wengi kifo cha mzee wetu ni sababu za kisiasa sababu alikua ni mzee wa mstari wa mbele kumpigania Esther Matiko hasa kwenye vijiwe vya kahawa. 
Ni uchungu usiosimulika aliokua nao ndg Matiko kwa kumpoteza mzee wetu mpambanaji. Sauti iliyosikika kutoka kwake wakati wa kutoa salamu za rambirambi ilikua ni sauti ya Machozi. Ni jambo lisilovumilika kabisa kwa mauaji ya ndugu zetu hawa. 
Siku ya juzi usiku wa saa mbili pia kijana wetu wa bodaboda anaejulikana kwa jina Mahalufu la Magoti alichomwa kisu tumboni na kupoteza maisha baada kukodiwa na watu wasiojulikana ambao wakijitambulisha kama ni Abiria. 
Team Matiko tumejumuika pia na vijana wa bodaboda kwa kuusindikiza msiba wa kijana wetu huyo aliye safirishwa kwenda kwao Musoma kwa mazishi.
Vijana wa Tarime lazima tujitambue na tusiwe ni watu wa kutumiwa kisiasa hasa kwenye mambo maovu kama haya ya kukatisha maisha ya binadamu wenzetu. Kwa mwendo huu nadiriki kusema kabisa tumezidiwa uwezo wa kufikiri na wanyama wa Mwituni.
Maisha yetu yataendelea kama kawaida baada ya uchaguzi huu. Sie sote ni ndugu, watoto wa baba mmoja. Lakini pia tukumbuke hata maandiko matakatifu yanasema Atakeua kwa upanga nae atauawa kwa upanga.
Mungu ibariki Afrika Mungu ibariki Tanzania Mungu ibariki Tarime
Bwana alitoa Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe".Anasema Peter Magwi Michael, Team Matiko Tarime Mjini.
Ndugu, Jamaa na Marafiki wakiuaga mwili wa aliekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema Kata ya Sabasaba, Tarime ukiagwa kwa ajili ya kwenda kupumzishwa.
Mgombea Ubunge Jimbo la Tarime Mjini (Chadema) Esther Matiko akizungumza wakati wa kuuaga mwili wa aliekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema Kata ya Sabasaba, Tarime kabla ya kwenda kupumzishwa.
Mwili wa aliekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema Kata ya Sabasaba, Tarime ukiagwa kwa ajili ya kwenda kupumzishwa katika Makaburi ya Lonsoti Wilayani Tarime.
Ndugu, Jamaa na Marafiki
BMG tunasisitiza kuwa Kumbuka kuna Maisha baada ya Uchaguzi, hivyo hakikisha harakati za uchaguzi hazivurugi amani iliyopo nchini.

No comments:

Powered by Blogger.