LIVE STREAM ADS

Header Ads

MKUMBO: UHAMISHO WA ASKARI ULIOFANYIKA MKOANI MWANZA UMELENGA KULIBORESHA JESHI.

Na:George Binagi-GB Pazzo wa Binagi Media Group
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Charles Mkumbo amefafanua kwamba mabadiliko ya askari wa Usalama barabarani yaliyofanyika hivi karibu Mkoani hapa, yalikuwa ni mabadiliko yenye lengo la kuimarisha zaidi utendaji kazi wa jeshi hilo.

Kamanda Mkumbo alitoa ufafanuzi huo hii leo mbele ya waandishi wa habari, kufuatia uvumi ulioenea mitaani kwamba askari hao walibadilishwa vitengo vyao vya kazi kutokana na utovu wa maadili kazini ikiwemo kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Amefafanua kwamba takribani askari 78 katika Wilaya saba za Mkoa wa Mwanza, walibadilishwa vitengo pamoja na vituo vyao vya kazi na kwamba mabadiliko kama hayo yataendelea kufanyika ndani ya vitengo vingine vya jeshi hilo.

Mabadiliko hayo yalihusisha Wilaya za Nyamagana, Ilemela, Kwimba, Magu, Sengerema na Misungwi ambazo utendaji kazi wa askari hao ulikuwa ukilalamikiwa na wananchi ambapo Wilaya ya Ukerewe haikuguswa na pangua pangua hiyo.
Katika hatua nyingine, Kamanda Mkumbo amebainisha kuwa, mvua iliyonyesha jumatatu ya wiki hii imesababisha kifo cha mtu mmoja pamoja na watu wengine zaidi ya 300 kukosa makazi ya kuishi, baada ya nyumba zao kuezuliwa na upepo mkali uliokuwa umeambatana na mvua hiyo.

Amemtaja aliefariki dunia kuwa ni Mzee Hollo Masamwa (80) Mkazi wa Kwimba, aliefariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba aliyokuwa akiishi.

No comments:

Powered by Blogger.