LIVE STREAM ADS

Header Ads

POLISI, CHADEMA WAVUTANA MKOANI MWANZA JUU YA SHUGHULI YA KUUAGA MWILI WA MAWAZO.

Kamanda wa Polisi Mkoani hapa Charles Mkumbo akiongea na wanahabari Ofisini Kwake (Hawako pichani).
Na:Binagi Media Group
Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza leo limepiga marufuku shughuli za kuuaga mwili wa aliekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Mkoani Geita Alphonce Mawazo, zilizokuwa zimepangwa kufanyika kesho katika Uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoani hapa Charles Mkumbo alisema kuwa jeshi hilo limechukua maamuzi hayo, kutokana na kuwepo kwa taarifa za zisizo njema kiusalama kwamba kuna baadhi ya vikundi vya watu vinatarajia kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kufanya fujo na hivyo kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.

Pia Kamanda Mkumbo aliitaja sababu nyingine kuwa ni uwepo wa mlipuko wa Ugonjwa wa Kipindupindu Mkoani Mwanza, ambao umesababisha jeshi hilo kupiga marufuku mikusanyiko ya aina yoyote inayoweza kuhatarisha usalama wa wananchi kwa mjibu wa taratibu za watalaamu wa afya.

Kutokana na sababu hizo, Kamanda Mkumbo alieleza kuwa ni vyema shughuli za Kuuaga mwili wa Marehemu Mawazo uliohifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando, zikafanyikia Mkoani Geita ambapo mazishi yanatarajiwa kufanyika.

Hata hivyo licha ya katazo hilo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kupitia Kiongozi wake wa Kanda ya Ziwa Victoria Tungaraza Njugu, kimebainisha kuwa shughuli za kuuaga mwili wa Marehemu Mawazo Mkoani Mwanza hazitaweza kuahirishwa na kwamba zitafanyika kesho kuanzia majira ya saa nne asubuhi kama zilivyopangwa katika ofisi za chama hicho Kanda ya Ziwa Victoria zilizopo Kona ya Bwilu Ilemela baada ya kunyimwa kibali cha kuutumia Uwanja wa Furahisha.

Kwa upande wake aliekuwa Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Mkoani Mwanza na kada wa Chadema Ezekiel Wenje, alisema kuwa marufuku hiyo ya jeshi la polisi haina mantiki yoyote kwa kuwa hofu ya kipindupindu Mkoani Mwanza haijaathiri shughuli zozote ikiwemo za kibiashara na ibada za dini kufanyika na kwamba viongozi wa Chadema wamepanga zoezi hilo kufanyika kwa amani.

Hofu ya uwepo wa mlipuko wa Ugonjwa wa Kipindupindu Mkoani Mwanza imethibitishwa na Mganga Mkuu Msaidizi Mkoa wa Mwanza Onesmo Rwakyendera ambae amebainisha kuwa mlipuko wa ugonjwa huo ulianza miezi miwili iliyopita na kwamba hadi sasa umewakumba watu 422 ambapo kati ya hao 18 wamepoteza maisha.

Alphonce Mawazo aliekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita alifariki dunia jumamosi iliyopita ya Novemba 14 majira yanayokadiriwa kuwa kati ya saa sita na saba mchana, baada ya kukatwa mapanga na watu wasiojulikana ambapo kuuawa kwake kunahusishwa na uhasama wa kisiasa na mazishi yake yanatarajiwa kufanyika wikendi hii katika Kijiji cha Chikobe Wilaya ya Busanda Mkoani Geita.
Kiongozi wa Chadema, Kanda ya Ziwa Victoria, Tungaraza Njugu akiongea na Wanahabari katika ofisi za Kanda.
Kiongozi wa Chadema, Kanda ya Ziwa Victoria, Tungaraza Njugu akiongea na Wanahabari katika ofisi za Kanda.
Agness Julius, Katibu wa BAWACHA Wilaya ya Ilemela akieleza kusikitishwa na maamuzi ya jeshi la polisi kuzuia shughuli za kuuaga mwili wa Mawazo Kufanyika Jijini Mwanza
Husna Amri Said ambae ni Mwenyekiti wa BAWACHA Wilaya ya Geita akieleza kupingana na kauli ya jeshi la polisi Mkoani Mwanza kuzuia mwili wa Mawazo kuagwa Jijini Mwanza
Julius Malifedha ambae ni Katibu wa Mwenezi Chadema, Wilaya ya Ilemela
Aliekuwa Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Mkoani Mwanza na kada wa Chadema Ezekiel Wenjea akiongea na Vyombo vya Habari.
Aliekuwa Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Mkoani Mwanza na kada wa Chadema Ezekiel Wenjea akiongea na Vyombo vya Habari.
Viongozi na Makada wa Chadema wakipinga tamko la jeshi la Polisi Mkoani Mwanza kuzuia shughuli za kuuaga mwili wa marehemu Mawazo
Tayari ulinzi umeimalishwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza ikiwemo jirani na zilipo ofisi za Chadema, Kanda ya Ziwa Victoria huku magari ya polisi na yale yenye maji ya kuwasha yakionekana katikati ya Jiji.

No comments:

Powered by Blogger.