LIVE STREAM ADS

Header Ads

TUHUMA ZA RUSHWA ZAWAKUMBA BAADHI YA WENYE NIA YA KUUSAKA UMEYA KATIKA HALMASHAURI YA MJI WA KAHAMA.

Na:Shaban Njia, Kahama
SAKATA la kumsaka Meya wa Halmashauri ya Mji wa Kahama Mkoani Shinyanga, limepamba moto ambapo baadhi ya Madiwani wapatao sita kati ya ishirini wanaounda Halmashauri ya Mji huo walioonyesha nia ya kuwania kiti hicho wameanza kutuhumiwa kwa kutoa rushwa ili kuipata nafasi hiyo.

"Wagombea hao wamekuwa wakishinda katika baadhi ya Mahoteli mbalimbali maarufu mjini hapa kwa lengo la kutoa rushwa za fedha pamoja na kuwanunulia wajumbe chakula na kuwagharamia nauli wajumbe wanaotoka kata mbalimbali zilizopo katika Halmashauri ya Mji huu". Alidokeza mmoja wa wakazi wa mjini Kahama kwa sharti la kutotaja jina lake.

Akizungumza kwa njia ya simu ya kiganjani, mmoja wa madiwani hao alisema “Ndugu mwandishi mimi hivi tunavyoongea nipo katani kwangu naendelea na kazi zangu, sielewi chochote kuhusu masuala ya rushwa yanayozungumzwa mitaani lakini  kuhusu kugombea ni kweli nimeonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo ya umea".

Diwani mwingine nae alisema “Kimsingi sisi kama Madiwani hatuwezi kumchagua mtu ambaye haijui Halmashauri hii pamoja na shughuli zake ambapo ukizingatia kuwa Halmashauri yetu imepanda hadhi na kuwa Halmashauri ya Mji  hali ambayo inahitaji kiongozi mwenye Elimu, Busara na mwenye kufuata maadili ili aweze kushirikiana vema na mkurugenzi”.

Sakata la kumpata Meya wa Halmashauri ya mji wa Kahama limekuwa gumzo kwa kuwa baadhi ya Madiwani kutoka kata mbalimbali wamekuwa wakifanya vikao visivyo rasmi huku rushwa za fedha zikidaiwa kusambazwa kwa baadhi ya wajumbe ambapo kila aliyeomba kiti hicho anafanya kila juhudi ili afanikiwe kukinyakua hatua ambayo baadhi ya wananchi wanaiomba Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU kuingilia kati.

No comments:

Powered by Blogger.