LIVE STREAM ADS

Header Ads

UMOJA WA WAENDESHA BODABODA MKOA WA MWANZA WATOA TAMKO KWA BODABODA WOTE NCHINI.

Na:George Binagi-GB Pazzo @BMG 
Umoja wa Waendesha pikipiki (Bodaboda) Mkoa wa Mwanza, umewahimiza Waendesha pikipiki wote nchini kusherehekea kwa amani Sikukuu ya Mwaka Mpya huku wakitimiza vyema majukumu yao kwa kufuata sheria na taratibu za Usalama barabarani.

Mwenyekiti wa Umoja huo Makoye Kayanda Bunoro ametoa rai hiyo wakati akizungumza na BMG (Binagi Media Group), ikiwa zimesalia siku tatu kuuaga mwaka huu wa 2015 na kuukaribisha mwaka mpya 2016.

“Niwaombe Waendesha pikipiki wote nchini washerehekee kwa amani shamrashara za kuukaribisha mwaka mpya, kuanzia mkesha huku wakitimiza majukumu yao kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuondokana na fujo zisizo za lazima ikiwemo kuchoma matairi barabarani kwa misingi ya kuukaribisha mwaka mpya 2016”. Amesema Bunoro.

Bunoro ameongeza kuwa ni vyema bodaboda wote wakatimiza majukumu yao kwa kutii sheria bila shuruti ikiwemo kutoendesha pikipiki huku wakiwa wametumia vilevi pamoja na kuzidisha abiria (mishkaki) ikizingatiwa kwamba bodaboda ni kazi halali hivyo waendane na kauli mbiu ya Mhe.rais Dkt.John Pombe Magufuli ya “Hapa Kazi Tu” katika kutimiza majukumu yao.

Pia amewahimiza watumiaji wengine wa barabara wakiwemo waendesha vyombo vya moto kama magari pamoja na watembea kwa miguu nao kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepukana na ajali zinazozuilika.

No comments:

Powered by Blogger.