+AUDIO. MACHINGA WAITADHARISHA HALMASHAURI YA JIJI LA MWANZA JUU YA BAJETI YAKE 2016/17.
Kushoto ni Mwenyekiti wa Muungano wa Machinga Mkoani Mwanza Said Tembo akiwatazama baadhi ya Vijana ambao ni Machinga Jijini Mwanza.
Halmashauri ya
Jiji la Mwanza imetakiwa kupanga vyema mikakati yake ya bajeti ya fedha katika
kipindi cha Mwaka 2016/17, kwa ajili ya Makundi ya Vijana na akina Mama, ili
kuyasaidia makundi hayo kujiajiri na hivyo kuondokana na tatizo la ukosefu wa
ajira.
Mwenyekiti wa Muungano wa Machinga Mkoani Mwanza Said Tembo,
ametoa kauli hiyo wakati akizungumzia changamoto ya ukosefu wa maeneo maalumu kwa
ajili Wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kwa jina la Machinga Jijini Mwanza,
jambo linalosababisha wafanyabiashara hao kuzagaa ovyo mitaani kinyume na
taratibu za Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Pamoja na mambo mengine, Moshi Maketa ambae ni Katibu Mkuu wa
Muungano wa Machinga Mkoani Mwanza, amesema kuwa Muungano huo unafanya kila
jitihada ili kuhakikisha Serikali inatoa mikopo kwa ajili ya Machinga, ili
kuwawezesha kujikwamua kiuchumi ikizingatiwa kwamba Sekta ya Machinga imekuwa
kimbilio la vijana walio wengi hapa nchini.
Jijini Mwanza, baadhi ya Machinga wanapaza sauti zao na kuiomba
Serikali kuiboresha Sekta hiyo, ili kuondokana na Changamoto zinazowakabiri
ikiwemo kukosa maeneo maalumu kwa ajili ya kufanyia biashara zao, hatua
inayosababisha wakumbane na kadhia mbalimbali ikiwemo kukabiliana na mgambo wa
Jiji.
Japo biashara ya machinga si biashara rafiki katika maeneo ya
katikati ya Jiji la Mwanza, lakini biashara hiyo imekuwa kimbilio la Vijana
walio wengi hususani kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambao kila kukicha hufika
Jijini Mwanza kwa ajili ya shughuli hiyo huku changamoto mpya ikiwa ni kuanza
kuwepo kwa idadi ya watoto wanaojiunga na biashara ya Machinga Jijini Mwanza na
hivyo kusababisha watoto hao kukosa haki yao ya kupata elimu.
BONYEZA HAPA KUSIKILIZA
BONYEZA HAPA KUSIKILIZA
Mmoja wa Machinga akifanya biashara katikati ya Jiji la Mwanza
Baadhi ya Machinga Jijini Mwanza eneo la Mataa
Baadhi ya Vijana Machinga Jijini Mwanza
Baadhi ya akina Mama wanaojishughulisha na biashara ya Kuuza Mihogo Jijini Mwanza
Mwenyekiti wa Muungano wa Machinga Mkoani Mwanza Said Tembo akizungumza na BMG kama ambavyo alinaswa katikati ya Jiji la Mwanza eneo la Mataa.
No comments: