LIVE STREAM ADS

Header Ads

MTANDAO WA ASASI ZA KUWAHUDUMIA WATU WENYE ULEMAVU NCHINI WAANZISHWA RASMI.

Judith Ferdinand, Mwanza
Kutokana na watu  wenye  ulemavu nchini, kukabiliwa na  changamoto mbalimbali ikiwemo elimu, asasi zinazojishughulisha  kutoa huduma na kutetea kundi hilo, zimeanzisha mtandao utakaosaidia kuongeza ufanisi katika kuwahudumia watu wenye ulemavu pamoja na kuihimiza serikali kuwasaidia watu hao.

Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa Mtandao wa Asasi zinazowahudumia Watu wenye  Ulemavu Tanzania (TDRC),  chini ya udhamini wa Karagwe Community Based Rehalitation Programmes (KCBRP), Walter Miya katika  mkutano mkuu wa umoja huo uliofanyika mkoani hapa.

Miya alisema, kupitia mtandao huo, itasaidia asasi hizo kuwa na ufanisi katika kutoa huduma  kwa walemavu  sambamba na kuelimisha  jamii juu ya kuwashirikisha, kutowanyapaa na kuwapa kipaumbele watu wa kundi hilo.

Pia alisema, itasaidia kuhimiza serikali kutoa huduma mbalimbali kwa walemavu  sawa na wengine ikiwemo suala la ajira, elimu na afya bora kwa kuboresha miundo mbinu , ambayo itakuwa rahisi na rafiki kwa kundi hilo.

Hata hivyo alisema, kupitia mtandao huo ambao umeanzia Kanda ya Ziwa, wataanzia mkoa wa Mwanza  katika suala la kupata takwimu za watu wenye ulemavu, ili  asasi hizo pamoja na serikali kufahamu idadi ya kundi hilo, na matatizo wanayokumbana nayo, jambo litakalosaidia kujua ukubwa wa changamoto na namna ya kukabiliana nayo.

Aidha aliiomba, serikali kutilia mkazo na kuhimiz jamii, wafanyabiashara, sekta binafsi kuwajali Walemavu kwa kuwashirikisha katika masuala mbalimbali ikiwemo ajira, elimu,michezo na uongozi, ili waweze kujitegemea.

Kwa upande wake Mlezi wa TDRC ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa KCBRP, Aggrey Mashanda alisema, lengo la mtandao huo ni kuleta ufanisi katika kutoa huduma kwa asasi hizo na kuongeza kasi kwa serikali kuweka mkazo wa kuwashirikisha walemavu kwenye shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Pia alisema, kwa sasa wanahudumia mikoa sita ya Kanda ya Ziwa, ila wanatarajia kuzifikia asasi zote nchini zinazojishughulisha na utoaji huduma kwa walemavu, ili  kusaidia kundi hilo kupiga hatua na kuacha kuwa tegemezi.

No comments:

Powered by Blogger.