LIVE STREAM ADS

Header Ads

VIONGOZI WA DINI KANDA YA KATI WATAKA AMANI UCHAGUZI MKUU

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

VIONGOZI wa dini mbalimbali kutoka Kanda ya Kati  wamewataka Watanzania kuendelea kulinda amani ya nchi na kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, wakisisitiza kuwa amani ni tunu na urithi wa thamani unaopaswa kulindwa na kila raia.

Wito huo umetolewa leo Oktoba 25, 2025, katika Kongamano la Amani lililofanyika jijini Dodoma, likijumuisha viongozi wa dini kutoka mikoa ya Dodoma na Singida.

Katika kongamano hilo, viongozi hao walijadili mada mbalimbali kuhusu umuhimu wa kupiga kura, historia ya chaguzi nchini na wajibu wa kila raia kulingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akitoa mada kuhusu umuhimu wa amani, Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa ya Kikristo Tanzania (CCT) Mkoa wa Dodoma na Askofu wa Kanisa la Mennonite Tanzania (KMT), Joseph Mtolela, amesema Tanzania imeendelea kuwa kisiwa cha amani katika kipindi chote cha kampeni, na hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha hali hiyo inaendelea hadi baada ya uchaguzi.

“Siku nne zijazo nchi yetu itakuwa kwenye mchakato wa uchaguzi. Tumekuwa na amani katika kipindi chote cha kampeni, na tunahitaji amani hiyo siku ya uchaguzi. Tushiriki kwa wingi, tuwe makini kuangalia chama au kiongozi atakayeleta amani, utulivu na usalama wa nchi,” amesema Askofu Mtolela.

Ameongeza kuwa amani ni zawadi kutoka kwa Mungu na ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa. 

“Mungu ameturuzuku amani, ni kipaji na kipawa. Tuna kila sababu ya kuitunza na kuilinda, kwani bila amani hakuna maendeleo, wananchi hawatakuwa salama, na tutakimbia nchi yetu wenyewe,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Mkoa wa Dodoma, Askofu Evance Chande wa Kanisa la Karmel Assemblies of God, amesema moyo wa uzalendo miongoni mwa Watanzania umeanza kupungua, na kuwataka viongozi wa dini kuungana kuhakikisha nchi inabaki salama.

“Sisi viongozi wa dini tuna jukumu kubwa kuhakikisha tunasimama kwenye nafasi zetu. Adui anapambana kuondoa amani, hivyo lazima tuamke, tushirikiane na Serikali, tuelimishane na hasa vijana wetu ambao mara nyingi hutumiwa vibaya. Tuwape elimu ya uzalendo na kuwaonya kutokuitumbukiza nchi kwenye migogoro,” amesema Askofu Chande.

Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro, amesema jukumu la kulinda amani liko mikononi mwa viongozi wa dini na waumini wao.

“Tatizo si sisi viongozi, bali baadhi ya waumini wetu wanaopoteza hofu ya Mungu na kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani. Tunapaswa kurudi kwao, kuwaonya na kuwaelimisha. Mwanzo wa moto ni cheche; tusiruhusu cheche hiyo iwake,” amesema Sheikh Nassoro.

Amesisitiza kuwa kushiriki uchaguzi ni sehemu ya kulinda amani. “Amani ni bora kuliko riziki. Jamii yoyote isiyoshiriki kupiga kura inajinyima haki ya kupata viongozi wanaokubalika, na matokeo yake ni vurugu. Ni jukumu letu kuwahamasisha watu kupiga kura kwa amani na kuchagua viongozi wenye maono ya kulinda mema ya taifa,” amesema Sheikh Nassoro.

Naye Askofu Zephania Mkuyu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Dodoma Magharibi, amesema suala la amani halina uhusiano wa kisiasa bali ni la kiroho, hivyo viongozi wa dini wanapaswa kuendelea kuhubiri amani na kuombea nchi.

“Kama viongozi wa dini tutasimama katika nafasi zetu, tutaona matokeo mazuri. Amani ni nguzo ya maendeleo ya kiroho, kijamii na kiuchumi,” amesema Askofu Mkuyu.

Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Alhaji Dkt. Mustapha Rajabu, amesema raia wote wanapaswa kuwa watiifu kwa viongozi wa dini na Serikali, na kuzingatia maelekezo yao kuhusu uchaguzi.

“Maandamano halali ni kwenda kupiga kura. Tarehe 29 wajitokeze kwa wingi, wachague viongozi watakaoliletea taifa maendeleo. Bila amani, familia zitaathirika na miundombinu kuharibika,” amesema Sheikh Rajabu.

Aidha, Mshauri wa Mufti, Alhaji Ismail Dawood, amewataka wananchi kutokuwa na hofu bali kujitokeza kupiga kura kwa amani, akisema:“Tusihofu vurugu, twendeni tukapige kura. Naomba waumini wote wakusanyike tarehe 29 kwenda kupiga kura kwa utulivu.”

Kongamano hilo lilihitimishwa kwa wito wa pamoja kutoka kwa viongozi wa dini wote waliohudhuria, wakiahidi kuendelea kuelimisha waumini wao kuhusu kulinda amani, kudumisha umoja wa kitaifa na kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu.   

No comments:

Powered by Blogger.