Fanya Mambo Haya Saba Ndani Ya Mwezi Huu Mpya.
Kwanza nakupa pongezi na hongera kwa kuwa pamoja katika
kumaliza Mwezi uliopita wote wa pili; ambao umeisha tangu hapo jana na sasa
tumeingia mwezi mpya wa tatu. Kumbuka Utukufu na Nguvu ni kwa Mungu aliyetupa
tena nafasi ya kuingia na kuuona tena mwezi huu mpya wa tatu tuliouingia hii
leo.
Na hivyo basi, leo napenda kukushirikisha mambo muhimu
ambayo ningependa uyafanye ndani ya mwezi huu mpya tunaouanza hii leo, na hasa
kama unahitaji kufanikiwa katika Malengo na ndoto yako uliyonayo ndani ya mwaka
huu 2016.
Kumbuka kila mwezi ndani yake ni mfano wa MIMBA ambayo
umeibeba wewe muhusika, na ambayo ni muhimu ujue unatakiwa mwezi usiishe
umekwishajifungua. Mimba ya kukusukuma kwenye kufanikisha malengo yako ya mwaka
mzima na hatimaye kufanikisha ndoto zako ulizonazo maishani mwako.
Suala sio kumaliza mwezi; Bali swali la muhimu la kujiuliza
ni Je, mwezi unapoisha unakuwa umefanikisha mambo mangapi yanayokupa nafasi ya
kutimiza ndoto yako nzuri uliyonayo maishani mwako? Hilo ni swali muhimu na la
msingi unalopaswa kujiuliza kila mara kabla na baada ya kuingia mwezi mwingine.
Kama hukubahatika kufanikisha mambo yako mengi ndani ya
mwezi uliopita; na yawezekana hadi sasa hujui utafanya nini. Nakusihi fanya
yafuatayo ili yawe sehemu kubwa ya kukusaidia kufanikiwa katika Malengo yako
ndani ya mwezi huu wa 3 tuliouanza hii leo, na ili usikosee tena kwa mara
nyingine kufikia malengo yako.
1:Tafuta jambo moja la kusimamia na kufanya mwezi huu
mzima.
Usijaribu kufanya kila kitu, utafeli kwa kufanya kila kitu.
Chagua jambo moja la kukusaidia kukupeleka katika kutimiza ndoto yako kiujumla
ndani ya mwezi huu. Hii itakujengea msingi mzuri na msimamo mwema wa kufikia
katika mafanikio makubwa unayoyahitaji.
Utafiti unaonyesha wazi watu wengi wenye kujaribu kufanya
kila jambo wanaloona kwao linamanufaa na kuacha kusimamia jambo moja; huwa
wanajikuta wanakosea mara kwa mara na hatimaye hata kushindwa kupata kitu
kikubwa walichokuwa wakitegemea kupata katika maisha yao.
2:Orodhesha watu si chini ya watano ambao unapaswa kukutana nao
haraka; ili kukusaidia katika kufikia malengo yako.
Hakuna mafanikio yanayoweza kufikika kama hayatojengwa
kwenye msingi wa kushirikiana na wengine. Unahitaji watu kila siku wa
kukusaidia kutimiza na kufikia ndoto yako kubwa uliyonayo maishani mwako. Kama
hautoona umuhimu wa kushirikiana na watu fahamu utakuwa unakosa nafasi kubwa ya
kufika haraka unapotaka kufikia.
Kwa kufahamu jambo hili zaidi; soma makala hii ya Unahitaji
watu sahihi wa kukubeba ili Kufikia katika Mafanikio makubwa itakupa ufahamu
zaidi.
3:Orodhesha kiwango cha rasilimali fedha na muda
unachokihitaji kila siku ili kufikia malengo yako ya mwezi huu mzima.
Usitumie muda wako na fedha yako vibaya; jiwekee bajeti ya
mwezi huu mzima; ili kukupa nafasi ya kutembea katika matumizi yaliyo ya muhimu
na ya lazima tu katika eneo hili la fedha na muda. Fedha na Muda ni rasilimali
muhimu sana ambazo zinaweza kuwa sehemu kubwa ya kumsaidia mtu kufikia katika
malengo mengi yanayohitaji rasilimali hizi.
Wewe binafsi unajua na kufahamu ya kuwa; karibu asilimia
kubwa ya malengo mengi ya watu au yako yanahitaji fedha na muda wa kutosha ili
kuweza kuyatimiza kwa uaminifu na ili uweze kuyafikia pasipo kigugumizi
chochote mbele yako. Ingawa bado utahitaji furaha na amani pia kama mambo
muhimu zaidi.
4: Badili muda wako wa kulala na kuamka.
Nakusihi uache tabia ya kuchelewa kulala, kwa kufanya hivyo
ni lazima utachelewa kuamka pia. Na hata kama si kuchelewa kuamka fahamu
unaweza kushindwa kufanya mambo yako vizuri katika siku yako inayofuata mbele
yako.
Jiwekee ratiba nzuri itakayokuongoza katika muda wako wa
kulala na kuamka mapema; ili uweze kujiendesha vizuri katika eneo hili na zaidi
sana ili uweze kujisaidia binafsi kwenye suala la afya na nguvu za kutimiza
ndoto yako. Kumbuka kuwa masaa yako unayoyatumia kulala ndio yanayoamua uwezo
wako wa kufanya kazi katika siku inayofuata. Kama hutolala usingizi wa kutosha
fahamu kesho yake itakuwa ngumu kufanya kazi vizuri kwa sababu utakuwa
umechoka.
Hivyo hivyo kwa upande wa pili. Kama utapata muda mrefu wa
kupumzika na kulala vya kutosha utakuwa umesaidia mwili na akili yako kujituma
zaidi katika siku inayofuata mbele yako. Ushauri wangu kwako ni kuwa, hakikisha
unatekeleza jambo hili kuanzia leo hii ili uweze kuona matunda mazuri juu ya
kazi zako na afya yako.
5:Zingatia kula chakula kilicho bora ambacho kinaweza kuwa
msingi mzuri wa kukufanya uwe na afya bora na nguvu ya kukusaidia katika
kutimiza ndoto na malengo yako uliyonayo.
Chakula unachokula ndio kinaamua afya yako na nguvu zako za
mwilini za kukusaidia katika kutimiza ndoto na maono yako mazuri uliyonayo.
Hakikisha unapangilia mlo wako na chakula unachotumia ili kukupa nguvu ya
kutumikia maono na kusudi la kuwepo kwako hapa duniani.
Tumia vyakula vizuri visivyo na mafuta mengi na vinywaji
visivyo na kokeini nyingi; usitumie vinywaji hivi mara kwa mara au uviache
kabisa, vinywaji kama vile soda, vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks),
nakadhalika; vinavyoweza kuwa hatari kwa afya yako na zaidi kukusababisha wewe
kushindwa kutumikia na kufikia malengo na ndoto zako ulizonazo.
6:Badili misimamo na tabia mbaya zisizofaa.
Tabia zinazokuzuia katika kufikia mafanikio makubwa. Zipo
tabia zinazoweza kuwa kizuizi kikubwa cha kumsababisha mtu kutokuweza kufikia
katika mafanikio makubwa ya kutimiza ndoto yake. Na zaidi sana watu wengi
wamekuwa na tabia hizi zinazokuwa kizuizi kwa upande wao wa kufikia mafanikio.
Fatilia makala hii ya Tabia 20 zinazozuia watu wengi kufikia
katika mafanikio makubwa utaelewa tabia hizo; soma kisha chukua hatua ya haraka
ya kubadilika kutoka katika tabia hizo ili uweze kufikia katika mafanikio yako
unayohitaji.
7:Soma vitabu 2 hadi 4 ndani ya mwezi huu.
Hakuna mafanikio makubwa nje ya kutoa muda wako kila siku
kwa ajili ya kujifunza mambo mapya yanayoweza kuwa msingi mzuri na mwema wa
kukusaidia kufikia maono na ndoto zako ulizonazo. Jiulize unapendelea kusoma
mambo gani; kumbuka kuwa yale unayoyasoma ndio yanayokujengea tabia tunayoiona
hii leo huku nje; jiulize swali kama unasoma na kufatilia zaidi mambo ya udaku;
Je, yanakusaidia vipi katika kufikia maono na ndoto yako uliyonayo moyoni
mwako?
Hivyo basi, hakikisha unasoma mambo mazuri au vitabu vyenye
maudhui mazuri ya kukujenga kitabia na kukusaidia katika kufanikisha ndoto yako
na kusudi la kuwepo kwako hapa duniani. Achana na kusoma habari za udaku tena
za maisha ya watu ambao asilimia kubwa wapo kwa ajili ya kuigiza zaidi, kuliko
kuonesha uasilia wa mafanikio yao ya kweli.
Hadi kufikia hapo nakutakia mafanikio mema ndani ya mwezi
huu tuliouanza; kumbuka ukitii na kufaata mambo yote niliyokuandikia hapo juu,
naamini utakula mema yote ya mwezi huu, na zaidi utaona mafanikio katika kila
jambo unaloligusa kulifanya.
Shukrani kwa ccbanttz Consultant.
No comments: