LIVE STREAM ADS

Header Ads

TAHARIRI: KWA NINI AGIZO LA IGP MANGU LINAPUUZWA.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu.
Na:Mhariri; Binagi Blog
Kwa muda mrefu kumekuwepo na malalamiko kwamba waendesha bodaboda nchini wamekuwa hawatii sheria za usalama barabarani, hali ambayo imekuwa ikisababisha ongezeko la ajali zinazoweza kuzuilika.

Hali hiyo ilimsukuma Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu mwishoni mwa mwezi uliopita, kutangaza Oparesheni kamata bodaboda wasiotii sheria za usalama barabara nchini nzima katika kikao kazi kilichowahusisha Maofisa Wakuu wa Polisi nchini wakiwemo Makanda wa Polisi Mikoa, Vikosi na Makao Makuu, kilichofanyika Jijini Dar es salaam.

“Pamoja na kuendelea kudhibiti uhalifu wa aina zote, natoa maelekezo kwa kila Mkoa kuhakikisha unaendesha oparesheni kali dhidi ya bodaboda ili kupunguza ajali zinazosababishwa na bodaboda ambao hawataki kufuata sheria na kanuni za usalama barabarabi”. Alisema IGP Mangu na kuainisha makosa yatakayosababisha bodaboda kukamatwa kuwa ni pamoja na Kubeba Mishikaki (abiria zaidi ya mmoja), Kutovaa kofia ngumu (helment) pamoja na kupita katika taa za barabarani huku taa nyekundu zikiwa zinawaka.

Baada ya kauli hiyo nilitegemea kuona utekelezaji ukianza mara moja katika mikoa yote nchini. Lakini hali inaonekana kwenda ndivyo sivyo. Jijini Mwanza, bodaboda bado makatazo yote ya IGP Mangu yanaendelea kuonekana. Mbaya zaidi ni pale Binagi Blog inaendelea kushuhudia bodaboda wakipita katika taa nyekundu huku wakiwa wamewabeba askari wa usalama barabarani.

“Wewe leo ungekoma. Yaani hawa sijui wakoje. Taa nyekundu zinawaka wao wanapita, tena ona amembeba askari.” Ilikuwa ni sauti ya malalamiko ya dereva wa daladala moja inayofanya safari zake za Maduka Tisa-Mzunguko Jijini Mwanza, baada ya kumkosa (nusra amgonge na gari) dereva bodaboda aliekuwa akipita katika mataa ya barabara ya Nyerere huku taa nyekundu zikiwa zimewaka, mbaya zaidi akiwa amembeba askari polisi kikosi cha usalama barabara (alikuwa amevalia sare).

Kwa hali hiyo, huko ni kumtusi IGP Mangu. Haiwezekani atoe agizo lakini bado agizo hilo lichukuliwe poa, mbaya zaidi na wale wenye jukumu la kusimamia agizo hilo (askari wa usalama barabarani). Binagi Blog inahoji “Agizo la IGP Mangu linatekelezwa au nalo ni kama maagizo mengine ambayo yamekuwa yakitolewa kwa minajiri ya kuwafurahisha wananchi”?

No comments:

Powered by Blogger.