LIVE STREAM ADS

Header Ads

MIAKA 20 TANGU KUZAMA MELI YA MV.BUKOBA, JE USAFIRI WA MAJINI NCHINI NI SALAMA?



Mei 21, 1996 taifa la Tanzania liligubikwa na msiba mkubwa ambapo kila mmoja kwa nanma yake aliguswa na msiba huo ambao uliyagharimu maisha ya mamia ya wapendwa wetu, baada ya meli ya Mv.Bukoba kuzama, hatua chache kabla ya kutua nanga mkoani Mwanza ikitokea mkoani Kagera.

Meli ya Mv.Bukoba iliyoundwa mwaka 1979 ikiwa na uwezo wa kubeba mizigo tani 850 na abiria 430 ilizama katika maji ya Ziwa Victoria Jijini Mwanza yapata umbali wa kilomita 30 kutoka ufukweni mwa maji.

Ajali hiyo ilisababisha zaidi ya watu 1,000 kupoteza maisha katika meli hiyo ambayo tangu kuundwa hadi kuzama kwake ilikuwa na umri wa miaka 17. 

Jambo la butwaa hapa ni idadi ya vifo na idadi ya abiria waliookolewa ukilinganisha na uwezo uwezo wa meli hiyo wa kubeba abiria wapatao 430.

Pengine tumezoea kwamba Mei 21 kila mwaka watanzania tunakumbuka kuzama kwa meli hiyo ambayo iliigeuza taswira ya mji wa Mwanza, kwani kwa waliokuwepo mwaka huo walipigwa na butwaa baada ya uwanja mkongwe wa Nyamagana ambao mara nyingi hutumika kwa shughuli za kimichezo, pale ulipogeuka na ghafla na kutapakaa maiti za wapendwa wetu, ama hakika inauma sana.

Wakati mwaka huu 2016 tunakumbuka tukio hili ambalo limeacha simanzi mioyoni mwetu, hebu tujiulize kwa pamoja kama ilivyo imani ya watalaamu wa masuala ya usafiri kwamba duniani kwamba usafiri wa majini ndio usafiri salama kuliko aina nyingine ya usafiri, Je kwa Tanzania imani hiyo ina mantiki yoyote kwamba vyombo vyetu vya usafiri wa majini ni salama?.

Lakini wakati tunatafakari suala hilo, pia tukumbuke kujiuliza sisi wenyewe bila kusubiri kusukumwa na mtu hususani wale wenye mamlaka ya kuleta matokeo chanya katika kuboresha hali ya usafiri majini ikiwemo Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini SUMATRA, kwamba tulijifunza jambo lolote kutokana na ajali hiyo ya Mv.Bukoba?

Na Kama kuna jambo tulijifunza, je tumefanikiwa kulifanyia kazi ipasavyo?. Je kuna hali yoyote ya uwajibikaji (kwa waliopewa dhamana ya kusimamia sheria) katika kuzingatia sheria za usafiri na usafirishaji wa majini na nchi kavu?. Je, tumekwisha jijengea hali ya kuchukua hatua za uokoaji pale tunapopatwa na majanga ya majini au nchi kavu?.

Lakini pia wapo waliohoji na bado wanaendelea kuhoji juu ya taarifa ama ripoti ya uchunguzi wa ajali hiyo ya Mv.Bukoba kama ulifanyiwa kazi ipasavyo? Lakini pia wakiwa bado wanaendelea kujiuliza, ni ajali ngapi za vyombo vya majini zimetokea tangu kuzama kwa meli hiyo? 

Hapo nadhani nawe unazikumbuka ajali kadhaa ambazo tayari zimekwisha kutokea na kuyagharimu maisha ya watanzania wengine ikiwemo ile ya Mv.Spice Ireland iliyotokea Septemba 10, 2011 katika mkondo wa Nungwi Kaskazini Unguja Zanzibar.

Lakini yote tisa, kumi ni sintofahamu iliyoibuka juu ya chanzo halisi cha ajali hiyo mbaya kuwahi kutokea hapa nchini. Wapo waliosema ilikuwa ni uzembe wa wakaguzi na waangalizi wa vyombo vya majini kwa maana ya mamlaka husika kama SUMATRA, wapo waliosema ilikuwa ni uzembe wa nahodha na timu yake na wapo waliosema chombo kilikuwa kibovu.

Lakini pia wapo waliodai chombo hicho kilikuwa kimebeba mizigo na abiria kuzidi uwezo wake na wapo waliodai kuwa abiria wenyewe walisababisha ajali hiyo kwani walilazimisha kupanda melini ilihali chombo kilikuwa kimejaa huku mrorongo huo ukihitimishwa na wale waliohusisha ajali hiyo na imani za kishirikina.

Sina nia ya kuandika hayo yote kwa lengo la kumtafuta wa kumtishwa lawama, laa hasha, ila lengo langu ni kuyaweka wazi hayo yote ili kila mmoja kwa namna anavyohusika na anavyoweza kusaidia ili kuhakikisha tunaeupakana na na ajali za majini kumbuka wahenga walisema tusiangalie tulipoanguka bali tuangalie tulipojikwaa.

Kumbuka watanzania wengi waliowapoteza ndugu, jamaa na marafiki zao na mmoja wao ambae alimpoteza mpendwa wake katika maisha yake ni mwanamitindo maarufu nchini, Flavian Matata ambaye alimpoteza mama mzazi pamoja na binamu yake.

Pamoja na watu wengine, Matata amekuwa na desturi ya kukumbuka tukio hilo kwa kufika jijini Mwanza katika eneo la Igoma ilipohifadhiwa miili ya waliopeza maisha katika ajali hiyo ya Mv.Bukoba.

Yapo mengi ya kuzungumza na kuandika lakini swali la kujiuliza ni moja tu, miaka 20 mwaka huu 2016 tangu kuzama meli ya Mv.Bukoba mnamo Mei 21,1996, je usafiri wa majini nchini ni salama ama tunasafiri kwa kudra za Mwenyezi Mungu? 

Nihitimishe kwa kusema ni jukumu la kila mmoja kwa kushirikiana na mamlaka husika ikiwemo SUMATRA kuhakikisha kuwa usafiri wa majini unakuwa usafiri salama nchini.

Imeandaliwa na George Binagi @Binagi Media Group
Kwa msaada wa mitandao mbalimbali.

No comments:

Powered by Blogger.