LIVE STREAM ADS

Header Ads

DC TESHA AWATAKA WAKULIMA KUTOKURUBUNIWA NA MAWAKALA WA PEMBEJEO ZA KILIMO.

Ikiwa Una Habari, Tukio, Picha, Maoni au Tangazo, Wasiliana Na BMG Kwa Nambari za Simu 0757 432694 Au Email binagimediagroup@gmail.com

Judith Ferdinand, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Mary Tesha, amewataka wakulima kutorubuniwa na mawakala wa pembejeo za kilimo za ruzuku kwa kupatiwa fedha kiasi.

Hii ni kutokana na baadhi ya mawakala wa pembejeo  za ruzuku  kuwarubuni wakulima kwa kuwapa  fedha kiasi na kutowapatia pembejeo mara baada ya kuwasainisha, ili serikali itambue kuwa ni waaminifu.

Tesha aliitoa kauli hiyo jana katika  ufungaji wa mafunzo ya   taaluma maalumu ya viuatilifu kwa ajili ya uendeshaji sahihi na salama wa biashara ya viuatilifu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu katika Kanda za Kitropiki (TPRI) Arusha, yaliyofanyika wilayani Nyamagana mkoani hapa.

Pia aliwataka wakulima kuwaelimisha wenzao juu ya pembejeo za ruzuku sambamba na kutoa ushirikiano wa kuwabaini mawakala hao, kwani serikali inatambua umuhimu wa sekta ya kilimo ndio maana waliamua kuchangia gharama za  pembejeo hizo,ili waweze kuvuna mazao mengi.

Hata hivyo, aliwaomba washiriki wa mafunzo hayo, kutumia elimu walioipata kwa vitendo na kuwaelimisha wengine, huku akiwataka  Ofisa Ugani  kutokukaa ofisini na badala yake watumie ujuzi walioupata kuelimisha wakulima vijijini juu ya matumizi sahihi ya viuatilifu sambamba na wafanyabiashara kufuata taratibu na sheria.

Aidha aliwataka wasajili Wa viuatilifu wawe waadilifu kwa kuhakikisha  wanasajili vile vinavyostahili kwani athari watakayowasababishia wananchi na taifa ni kubwa.

Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo ya  Udhibiti wa Visumbufu na Viuatilifu toka (TPRI) Arusha Habib Mkalanga alisema, mafunzo hayo yamelenga kuwasaidia Ofisa Ugani,wakulima wawezeshaji na wafanyabiashara kutumia kwa usahihi na kuwaelekeza namna ya kugundua viuatilifu ambayo siyo sahihi na vimekwisha muda.

Naye Ofisa Mfawidhi, Kitengo cha Huduma ya Afya ya Mimea Mwanza Doroth  Lusheshanija alisema, zaidi ya washiriki 68 kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera, Simiyu, Geita, Tabora, Shinyanga, Kigoma, Pwani, Mara  na Singida wamepatiwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu ambavyo ndio msingi katika kilimo ambacho ndio uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.

Vilevile  Ofisa Ugani wa  wilaya ya Kahama Anthony Masome alisema, kupitia mafunzo hayo wamejengewa ujasiri na kuongeza ujuzi ambao watatumia kuwaelekeza wakulima vijijini namna ya kutumia kwa usahihi viuatilifu, ili kuondokana na malalamiko yaliyopo.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Kiyunga Heri alisema, wamewezeshwa kufahamu matumizi sahihi ya viuatilifu sambamba na elimu itakayowawezesha wakulima kutumia bila kuathiri mazingira.
Soma mwanzo wa habari HAPA 

No comments:

Powered by Blogger.