LIVE STREAM ADS

Header Ads

RAIS MAGUFULI ASHAURIWA KUHUSU MIKUTANO YA VYAMA VYA SIASA.

Ikiwa Una Habari, Tukio, Picha, Maoni au Tangazo, Wasiliana Na BMG Kwa Nambari za Simu 0757 432694 Au Email binagimediagroup@gmail.com

Ukimsikiliza vizuri Mhe.Rais John Magufuli unaona ni yake ya dhati ya kuondoa kero zilizokuwa mwiba kwa serikali ya CCM na hata kufifisha umaarufu na imani ya wananchi kwa chama hiki kikongwe barani Afrika.

CCM, iliporomosha umaarufu wake kutokana na kugubikwa na tuhuma za rushwa,ilipata wakati mgumu kuanzia bungeni mpaka nje ya bunge kutokana na kila kukicha kuibuka kwa kashfa nyingi za rushwa, ndani ya bunge CCM ilikuwa na kibarua kigumu cha kupangua tuhuma za rushwa dhidi ya serikali yake, nje ya bunge CCM pia ilikuwa na kibarua kigumu cha kupangua tuhuma za rushwa.

Ilifika mahali CCM ilikuja na kampeni ya ya kujivua gamba, kampeni ya mawaziri mizigo na kampeni ya mwisho mwisho iliyoongozwa na katibu mkuu Abdulahman Kinana aliyezunguka nchi nzima kukiimarisha chama,alilala mijini na vijijini, alikula na kufanya kazi na wananchi, aliituhumu serikali kama walivyokuwa wakiituhumu wapinzani ili kurejesha imani ya wananchi kwa chama.

Haikuwa rahisi kwa CCM kurejesha uimara wake kwa wana CCM, kama siyo kampeni kali iliyoongozwa na Kinana, aliyejaribu kuwaaminisha watanzania kuwa Chama na serikali ni vitu viwili tofauti, alionesha uchafu na udhaifu unaolalamikiwa hauna uhusiano na chama.

Vyama vya upinzani, vilitumia udhaifu wa serikali ya ccm kushindwa kudgibiti rushwa kuandaa mikutano na maandamano makubwa karibu kila nchi,wakiwa na ajenda ya kupinga ufisadi,kati ya mwaka 1985 mpaka 1995 nchi ilikutana na migomo mingi kutokana na hali ngumu ya maisha na utofauti wa kipato kati ya aliyenacho na asiye nacho.

Hali ngumu ya maisha, utofauti wa kipato, rushwa na ufisadi ndiyo ulikuwa msingi wa maandamano na mikutano isiyokwisha ya vyama vya upinzani nchini, vyama vilizunguka nchi nzima kuwaeleza wananchi udhaifu wa serikali kukabiri rushwa na kuboresha maisha ya wananchi wake.

Kama si maandamano, mikutano, na ujasiri wa baadhi ya wanasiasa na vyombo vya habari, nadhani rushwa ingekuwa imeshaitafuna nchi, nakumbuka jinsi Zitto Kabwe alivyofukuzwa bungeni baada ya kutuhumu uwepo wa wizi kwenye mikataba ya madini, kufukuzwa kwake kulizalisha mikutano na maandamano chini ya Chadema wakiueleza umma udhaifu kwenye mikataba ya madini.

Nakumbuka jinsi Dkt.Wilbroad Peter Slaa wakati huo akiwa mbunge, alivyokuwa akisumbuana na spika Sitta kuhusu sakata la Dowans, EPA, Meremeta, n.k.

Dkt.Slaa aliiyumbisha serikali bungeni kila liposimama kuchangia bungeni, kuzuiwa kwa Dkt.Slaa kuyasema hayo bungeni, kuliwapa nafasi chadema kuhamisha ajenda hizi nje ya bunge na kuandaa mikutano na maandamano kila kukicha.

Nakumbuka jinsi David Kafulila alivyojaribu kuzunguka nchi nzima kueleza sakata la ESCROW, nakumbuka jinsi kamati ya Dkt.Mwakyembe ilivyozunguka nchi nzima kusaka ukweli juu ya sakata la Richmond.

KWA NINI NAYAKUMBUSHA HAYA?
Nayakumbusha ili kuweka sawa hili linaloibuka sasa,ukiwasikiliza baadhi ya watanzania na hata Mhe.Rais, wanalalamika kuwa nchi hii imekuwa masikini kwa sababu watu hawafanyi kazi, wanakalia maandamano na mikutani ya kisiasa, Rais kila siku analalamika kuwa sasa ni wakati wa kufanya kazi, watu waachanae na siasa.

Kwanza nimpongeze sana Rais kwa kuhimiza watu kufanya kazi na kuacha uvivu, ni kweli taifa hili haliwezi kwenda mbele kama hatutajenga utamaduni wa kufanya kazi, lakini Rais afahamu kufa kwa viwanda, umasikini, miundombinu kuharibika, hakujasababishwa na maandamano na mikutano isiyo na ukomo kutoka kwa vyama vya siasa vya upinzani.

Richmond, Meremeta, EPA, Deep Green, ESCWOR, Dowans, kuuzwa kwa benki kwa bei ya kaptula, mikataba mibovu ya madini, twiga kubebwa kwa ndege, wafanyakazi hewa, n.k hakujasababishwa na maandamano na mikutano ya vyama vya siasa, haya yamesababisha maandamano na mikutano ya vyama vya siasa isiyo na kikomo katika miaka iliyopita.

Watu waliandamana kwa sababu kulikuwa na rushwa karibu kila eneo, uchumi wa nchi ulikuwa unaporomoka kila siku, huduma za jamii zilikuwa duni kila kunapokucha, miundo mbinu ilikuwa inakufa kila siku, umasikini ulikuwa unatamalaki, watu walikuwa wakikata tamaa, kwa namna fulani namuona rais kaamua kujibu kero nyingi, zilizosababisha maandamano na mikutano yenye hotuba kali kutoka kwa wapinzani.

USHAURI KWA RAIS.
Njia pekee ya kuvifanya vyama vya siasa kuachana na maandamano na mikutano ya hadhara isiyo na kikomo, ni kuhakikisha yale yote yaliyokuwa kero kubwa kwa wananchi na kufifisha umaarufu wa CCM unayashughulikia, rushwa, watumishi hewa, umasikini, ukosefu wa ajira,ufisadi, ukiyashughulikia haya, utabadili kabisa aina ya siasa nchini, hata wapinzania watabadili aina ya siasa zao.

Rais haitaji kutumia muda mwingi, kwenye majukwaa kuwaonya wapinzani kuwa atawashughulikia kama wataandamana na kufanya mikutano ya hadhara, tatua rushwa, rejesha viwanda, ondoa ufisadi, rejesha reli ya kati, paisha nchi mpaka ifikie kuwa nchi ya ulimwengu wa kati, huitaji kuwabana wapinzani wako.

Nadhani rais una nafasi na uwezo mkubwa wa kurejesha imani na mvuto wa chama cha mapinduzi bila kuwazuia wapinzani wako, rais unaongoza watu waelewa sana, ukitatua kero zao, ukiendesha nchi kwa kuondosha kero zao huku ukitembea na ajenda ya wananchi.

Viache vyama vya siasa vifanye kazi kwa mujibu wa sheria, tembea na ajenda ya wananchi wanaochukia umasikini, rushwa na ufisadi, wanataka miundo mbinu bora, wanataka kuona maisha yanakuwa nafuu, ukiwafanyia hivi, hutawaona wanaandamana na kwenda kufurika kwenye mikutano ya vyama vya siasa, na utaona jinsi wapinzani wanavyotafuta njia nyingine ya kukikabiri chama cha mapinduzi, hayo unayoyapinga, hayapo kisheria, kama serikali itasimamia utamaduni huu wa kuendesha siasa, itakuwa inatengeneza maswali mengi sana, kwa nini hivi wakati sheria ya vyama vya siasa na katiba zinatoa nafasi kwa hayo yanayoliliwa na wapinzani?

Rais umeanza vizuri sana kwa kujibu baadhi ya kero za wananchi, usiteleze kwa kuamua kupambana na vyama vya upinzani.

Wasalaam, Mungu ibariki Tanzania.
Dotto Bulendu
Mhadhiri/Mwanahabari

No comments:

Powered by Blogger.