LIVE STREAM ADS

Header Ads

WAJASIRIAMALI WAENDELEA KUPEWA MAFUNZO JIJINI MWANZA.

Ikiwa Una Habari, Tukio, Picha, Maoni au Tangazo, Wasiliana Na BMG Kwa Nambari za Simu 0757 432694 Au Email binagimediagroup@gmail.com

Judith Ferdinand, Mwanza
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TAN TRADE), ikishirikiana na Taasisi ya Teknokojia Dar es salaam ( DIT) tawi la Mwanza, wanaendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo yenye lengo la kuendeleza sekta ya ngozi nchini.

Hayo yalisemwa  juzi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAN TRADE Edwin Rutageruka katika  hafla za ufungaji wa mafunzo ya utengenezaji wa mipira ya miguu kwa wajasiriamali wadogo yaliyofanyika DIT wilayani Ilemela mkoani hapa.

Rutageruka alisema, mafunzo hayo ni muhimu yenye lengo la kuendeleza sekta ya viwanda  kuanzia vidogo vya vijijini, vitongoji,mjini mpaka vya kati na vikubwa kupitia sekta ya ngozi.

Aidha alisema, mamlaka hiyo inawajengea uwezo na kuwaendeleza wazalishaji wadogo wakiwemo  wa bidhaa za ngozi kwa kutekeleza mpango wa kutoa mafunzo, kliniki ya biashara na huduma za ushauri kwa jamii ya wafanyabiashara.

Hata hivyo alisema, wameamua kuandaa ngozi bora kwa kutoa mafunzo kuanzia kwenye uchangaji, uchunaji huku wakishirikiana na DIT Mwanza, hii ni baada ya kufanya utafiti  katika mikoa ya Mwanza, Arusha na Kilimanjaro na kubaini fursa kubwa ingawa changamoto iliyojitokeza ni ya ubora wa ngozi.

Pia alisema, katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kuanzia aprili mwaka huu mpaka sasa wameisha toa mafunzo kwa wachuna ngozi 150, kutengeneza viatu kwa watu 50 na mipira ya miguu 16, hivyo wanatarajia kuendelea kutoa mafunzo nchi nzima.

Vilevile alisema, kutokana na umuhimu wa sekta hii katika kujenga uchumi wa viwanda, alimuomba Mkuu wa  Mkoa wa Mwanza John Mongella kutatua changamoto zinazokabili ubora wa ngozi katika mkoa wake, hususani kwa wafugaji,wachunaji na watengeneza bidhaa.

Kadhalika aliongeza kwa kumuomba Mongella  kuzielekeza halmashauri zote kuanzia mwaka  ujao wa frdha kutenga fedha kuanzia asilimia 5  ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuanzisha mfuko maalum na kuvikopesha vikundi vya wazalishaji wa bidhaa za ngozi, ili kutatua changamoto ya mitaji kwa wajasiriamali hao.

Naye Mongella aliwapongeza TAN TRADE na DIT kwa kuandaa mafunzo hayo, ambayo ni utekelezaji kwa vitendo wa dhana ya mpango wa pili wa maendeleo miaka mitano  na msisitizo wa serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ili kuchochea mageuzi ya uchumi hatimaye kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Pia alisema,sekta ya ngozi inapewa kipaumbele na  uongozi wa  mkoa,ili kuhakikisha kwamba inaimarika zaidi kwa kutoa mchango katika kuwaondolea wananchi umaskini, kuongeza ajira na kukuza pato la taifa kwa ujumla.

Aliongeza kwa kusema kuwa ngozi ni miongoni mwa sekta zenye fursa nchini kutokana na idadi ya mifugo iliyopo na masoko ya bidhaa hizo ndani na nje ya nchi ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha DIT Albert Mnari alisema, kupitia  ofisi ya mkoa anaiomba serikali kusaidia upatikanaji wa kiwanda cha usindikaji na uchakataji wa ngozi ghafi na utengenezaji Wa bidhaa za ngozi  kwa minajili ya uzalishaji na ufundishaji mafunzo kwa vitendo kwa mkoa, kanda na taifa.


Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Nestory  Mkumbi alisema wanaunga mkono juhudi za serikali za kufufua viwanda, kwani  wao  wameanza na ngozi hivyo wanaomba kutafutiwa soko  la uhakika ndani na nje ya nchi kwa ajili ya bidhaa watakazo zalisha.

No comments:

Powered by Blogger.