LIVE STREAM ADS

Header Ads

TFDA Kanda ya Ziwa yafunga duka la kuuza dawa za binadamu la Magira Phamarcy Jijini Mwanza.

Ikiwa Una Habari, Tukio, Picha, Maoni au Tangazo, Wasiliana Na BMG Kwa Nambari za Simu 0757 432694 Au Email binagimediagroup@gmail.com

Na.Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Ofisi ya Kanda ya Ziwa imelifunga kwa muda duka la kuuza dawa za binadamu la Magira Phamarcy ili kupisha upelelezi baada ya kukutwa likiuza dawa bandia na dawa zisizo na usajili kinyume na sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219 ya mwaka 2003.

Katika ukaguzi uliofanyika katika duka hilo liliko katika makutano ya Mtaa wa Nkuruma na Uhuru Jijini Mwanza aina tatu za dawa bandia zilikutwa zikiuzwa.

Mkaguzi wa Dawa wa TFDA Kanda ya Ziwa Mtani Njegere alizitaja dawa bandia zilizokamatwa kuwa ni  makopo 20 ya dawa bandia za kutibu malaria aina ya Quinine Sulphate BP toleo namba 150002 iliyotengenezwa Mwezi Mei 2015 na ambayo tarehe ya mwisho wa matumizi ni April 2019 inayodaiwa kutengenezwa na kiwanda cha Shelly Pharmaceuticals cha Jijini Dar es Salaam na makopo 24 ya dawa bandia za Asprin (vidonge) toleo namba 66436 inayodaiwa kutengenezwa mwezi Mei 2016 ambayo mwisho wake wa matumizi ni Aprili 2019.

“Tuligundua kuwa dawa aina ya Quinine Sulphate BP ni bandia kwa sababu taarifa juu ya lebo zilikuwa zinatofautiana na herufi (font Size) katika tarehe ya kutengeneza na matoleo zilikuwa tofauti jambo ambalo si utaratibu wa viwanda vinavyofuata taratibu sanifu za kutengeneza dawa (GMP) kama Shellys. Kwa upande wa Asprin alama muhimu katika lebo zinazotambulisha dawa kuwa ni ya kiwanda cha Labs & Allied hazikuwepo. Dawa kama hii pia iliwahi kukutwa katika duka moja huko mkoani Mara” alisema.

Mtani alizitaja dawa bandia nyingine zilizokutwa katika duka hilo kuwa ni vichupa 30 vya dawa ya Penicillin G (Sodium benzylpencillin) inayodaiwa kutengenezwa na kiwanda cha CSPC Zhongnhuo pharmaceutical for Dawa Limited na kopo moja la dawa ya caredomet (indomethacin) inayodaiwa kutengenezwa na kiwanda ch Shanxi Xinxintong Co. L TD cha nchini China.

Aidha Mtani alisema kuwa mmiliki wa duka hilo alishindwa kuwaeleza wakaguzi mahali aliko nunua  dawa hizo bandia na hivyo duka lake kufungwa  na kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219 ya mwaka 2003. “Ni utaratibu wa kitaalamu kutunza kumbukukumbu za manunuzi ya dawa. Kwa kuwa hakutuonesha stakabadhi za manunuzi zinazoonesha alikopata hizi dawa bandia ni wazi kuwa amezinunua katika eneo lisilo rasmi kinyume na taratibu” alisema.

Mbali na kukutwa na dawa bandia pia duka hilo lilikutwa na dawa ambazo hazikuwa na usajili kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA). Mtani alizitaja dawa hizo kuwa ni Folic Acidi (Tablets), Ampimed (Ampicillin inj), Chlorpromazine inj), Adrenaline injection na Zithromax (Azithromax).

No comments:

Powered by Blogger.