LIVE STREAM ADS

Header Ads

Tantrade kuwaunganisha wazalishaji wa bidhaa za viungo kwenye na soko la ndani

Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.

Judith Ferdinand,Mwanza
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), inaandaa mpango utakaowawezesha wazalishaji wa bidhaa za viungo(Spices) nchini,kupata soko endelevu na uhakika la ndani.

Soko hilo  la uhakika ni kupitia  kiwanda cha VEGETA PODRAVKA LTD kilichopo mjini Bagamoyo.

Hayo yameelezwa kwa njia ya simu  na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade  Edwin Rutageruka hivi karibuni,   baada ya kutembelea na kufanya mazungumzo na viongozi kiwanda hicho.

"Taarifa nilizozipokea ni kwamba kiwanda kina uwezo wa kuzalisha tani 2.5 za bidhaa za viungo  kwa siku, lakini  wanazalisha chini ya asilimia 50 kutokana na changamoto za malighafi toka ndani ya nchi pamoja na  masoko,hivyo imepelekea kiwanda hicho kuagiza malighafi toka nje ya nchi kutokana na kukosekana kwa viungo vyenye ubora unaotakiwa," alisema Rutageruka.

Hata hivyo alisema, wamekubaliana na uongozi wa kiwanda,waunganishwe na wazalishaji wa bidhaa kama tangawizi, pilipili manga, iliki, mdarasini na nyinginezo ambazo zimesindikwa na zimethibitishwa na TBS na TFDA kuwa zinakidhi viwango.

  Tanzania ni moja ya nchi Barani Afrika zinazozalisha bidhaa za viungo kwa wingi lakini wazalishaji wengi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ubora wa bidhaa  na uwezo mdogo wa uzalishaji.
Zanzibar inafahamika duniani kama "Spices Island" kutokana na uzalishaji wa viungo kwa wingi, ambapo mikoa mingine nchini  inayozalisha viungo  kwa wingi ni pamoja na Morogoro, Tanga,Kigoma,  Kilimanjaro, Mbeya na Kagera.

"Katika mpango huu tutazishirikisha Taasisi tunazofanya nazo kazi kwa karibu ikiwemo TBS, TFDA na SIDO,kuhakikisha wazalishaji wanapata mafunzo ya ubora wa bidhaa zao na vifungashio ili waweze kuzalisha bidhaa zinazokubalika na kiwanda  hicho na kuuza katika soko hilo la uhakika.
Aidha alisema, katika ushirikiano wao na taasisi hizo, wameishatoa mafunzo kwa wakulima wa viungo 202 waliopo mkoani Morogoro.

Kadhalika alisema,kiwanda hicho  ni moja ya viwanda bora vya bidhaa za viungo katika ukanda  wa Afrika, kimezinduliwa Desemba 2016, ikiwa ni kuitikia wito wa serikali ya awamu ya tano ya  kuifanya Tanzania  ya viwanda ifikapo mwaka 2025.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uwezeshaji wa VEGETA PODRAVKA LTD Bw. Archard Ngemela alitoa wito kwa wakulima wa bidhaa za viungo nchini kuongeza uzalishaji, kusindika bidhaa zao na kuzingatia ubora.

"Kiwanda chetu kikishaingia  mkataba na mzalishaji kinahitaji kuwa na uhakika wa kupata malighafi kwa mwaka mzima" alisema Ngemela.

No comments:

Powered by Blogger.