Pumzika kwa amani mzee Majuto
Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.
Na Emmanuel Shilatu
Nimepokea
kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za msiba wa msanii nguli na bingwa wa
tasnia ya sanaa za uigizaji na vichekesho, Amir Athuman almaarufu "King
Majuto" kilichotokea usiku wa Agosti 8, 2018 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili
alipokuwa akipatiwa matibabu kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.
Kifo hiki
kimenikumbuka miaka ile ya zamani alipoanza kuwika na msemo wa hamsini, hamsini
mia akiwa na muigizaji mwenzake mkongwe marehemu mzee Small. Kwa
wasiomjua vyema King Majuto alizaliwa mwaka 1948 jijini Tanga na kusoma shule
Msambwini mkoani Tanga. Alianza kuigiza mwaka 1958 akiwa na umri wa miaka tisa
akiigiza katika majukwaa.
Mzee Majuto
maarufu kama King Majuto ni mtunzi, muigizaji, mwandishi wa mswada. Pia mzee Majuto
ni muigizaji wa kwanza kuandaa kazi zake katika mikanda na kuuza akiwa na
Tanzania Film Company ( TFC). Kwa sasa
King Majuto ni mwigizaji mwenye mashabiki wengi kutokana maonyesho mbalimbali,
vichekesho vyake aliyoshiriki. King
Majuto ni kipaji halisia cha kuzaliwa cha uchekeshaji kuwahi kutokea hapa
nchini.
Wenzake walikuwa kina Mzee Jongo, Hamis Kitambi, Fundi Said (Mzee
Kipara) na Mama Haambiliki. Msiba huu ni
majonzi makubwa sana kwa familia, wasanii, tasnia ya filamu nchini, wapenzi wa
kazi zake za sanaa na Taifa kwa ujumla. Daima tutakukumbuka kwa ufundi, ustadi
wa uigizaji wako, vituko vyako, tabasamu lako, upendo wako kwa kila mtu.
Pumzika kwa amani mfalme na bingwa wa
vichekesho wa kipindi chote hapa nchini mzee "King Majuto". Inna
lillaahi wainna ilaihi raajiuun.
No comments: