LIVE STREAM ADS

Header Ads

RC Mongella aridhishwa na ujenzi wa shule ya sekondari JUMAKI

Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.

Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe. John Mongella akizungumza kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa shule ya Sekondari ya JUMAKI iliyopo Kata ya Lwanhima Jijini Mwanza.

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe. John Mongella ameridhishwa na ujenzi wa shule ya sekondari JUMAKI iliyopo katika Kata ya Lwanhima Jijini Mwanza, na kuhimiza ujenzi wa shule hiyo ukamilike kwa wakati ili wanafunzi waanze masomo.

Mhe. Mongella ametoa kauli hiyo Septemba 09, 2018 alipokuwa mgeni rasmi kwenye harambee ya kuchangisha fedha kiasi cha shilingi milioni 200 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa shule hiyo ambayo itakuwa ikipokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

Hata hivyo Mhe. Mongella alishauri uongozi wa shule hiyo kujenga mabweni kwa ajili ya wanafunzi watakaokuwa wanasoma shuleni hapo ili kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu hatua ambayo itawasaidia kujikita zaidi kwenye masomo huku akiongeza kwamba shule ziko nyingi hivyo suala la ubora wa elimu lazima lizingatiwe ili kuendana na ushindani.

Naye Mangi Mkuu (Mwenyekiti) wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kilimanjaro (JUMAKI) inayomiliki shule hiyo, Sir Sisha Swai alisema itakuwa ya mchepuo wa sayansi ili kuendana na kasi ya Mhe. Rais Dkt. John Magufuli ya kuwa na Tanzania ya viwanda.

Alisema hadi sasa majengo yaliyokamilika ni madarasa manane, jengo la utawala, vyoo, vyumba vya waalimu na ujenzi wa maabara ambao uko kwenye hatua za awali, yakigharimu shilingi milioni 340 huku zikihitajika shilingi milioni 400 ili kukamilisha ujenzi huo ambapo matarajio ni kuanza kupokea wanafunzi Julai 2019.

Aliomba serikali kusaidia kutatua changamoto ya ubovu wa barabara pamoja na ukosefu wa maji shuleni hapo kwani licha ya kuunganishwa na mfumo wa maji, bado hakuna maji ya ukakika.

Jumuiya ya Maendeleo ya Kilimanjaro (JUMAKI) ilianzishwa mwaka 1992 ambapo hadi sasa ina wanachama 2,840 ambao ni waliozaliwa, kuoa ama kuolewa mkoani Kilimanjaro lakini wanaishi mkoani Mwanza.
Mangi Mkuu (Mwenyekiti) wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kilimanjaro (JUMAKI) inayomiliki shule ya sekondari JUMAKI, Sir Sisha Swai akizungumza wakati wa harambee hiyo
Mangi Mkuu wa JUMAKI, Sir Sisha Swai (kushoto) akimkabidhi Katiba ya jumuiya hiyo Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe. John Mongella (kulia) kumkaribisha kujiunga na jumuiya hiyo
Baadhi ya wana JUMAKI waliohudhuria harambee hiyo
RC John Mongella (katikati mbele), viongozi na wanachama wa JUMAKI wakitembelea maeneo mbalimbali ya shule ya sekondari JUMAKI
Wana JUMAKI wakishiriki harambee ya kuchangia ujenzi wa shule
Mgeni rasmi akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa JUMAKI
Tazama BMG Online Tv hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.