Mawaziri wa sekta ya Kilimo wakutana Jijini Dodoma kujadili utekelezaji wa ASDP II
Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.
Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na walemavu Mhe
Jenista Mhagama (Mb) akizungumza jambo
wakati akifungua kikao cha Mawaziri wa sekta za kilimo juu ya utekelzaji wa
Mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II) leo tarehe 10
Octoba 2018.
Kutoka kushoto ni waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya
makazi Mhe Willium Lukuvu (Mb), Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba
(Mb) na Naibu waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji wakifuatilia kwa
umakini kikao cha Mawaziri wa sekta za kilimo juu ya utekelzaji wa Mpango wa
kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II).
Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akieleza
umuhimu wa kuanza haraka utekelezaji wa ASDP II wakati wa kikao cha Mawaziri wa
sekta za kilimo juu ya utekelzaji wa Mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo awamu
ya pili (ASDP II).
Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Mhe Willium
Lukuvu (Mb), akisisitiza jambo wakati wa kikao cha Mawaziri wa sekta za kilimo juu
ya utekelezaji wa Mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II).
Kulia ni Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba.
Naibu waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji akieleza
utayari wa ushiriki wa wizara yake wakati wa kikao cha hicho.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,
Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhe Jenista Mhagama (Mb) akizungumza jambo wakati akifungua kikao cha
Mawaziri wa sekta za kilimo juu ya utekelzaji wa Mpango wa kuendeleza sekta ya
kilimo awamu ya pili (ASDP II).
Na Mathias Canal,
WK-Dodoma
Mawaziri wa wizara za sekta ya kilimo leo tarehe 10 Octoba
2018 wametuama kwa masaa kadhaa Mjini
Dodoma katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kujadili kwa kina kuhusu
maandalizi ya utekelezaji wa Mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili
(ASDP II).
Wizara washirika katika kutekeleza ASDP II ni pamoja na
Wizara ya kilimo, Wizara ya mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda, Biashara, na
Uwekezaji Wizara ya Maji, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi, na
Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
Utekelezaji wake utachagizwa pia na Wabia wa maendeleo, Sekta
binafsi, Taasisi zisizo za kiserikali, Wakulima, Wafugaji na Wavuvi.
Mawaziri hao wakiongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Waziri wa
Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na walemavu Mhe Jenista Mhagama (Mb)
wameridhia kwa pamoja kuanza haraka utekelezaji wa mradi huo wa ASDP II ambao
utakuwa chachu ya ukuzaji wa uchumi kupitia kilimo.
Majadiliano hayo yalijikita zaidi kujadili mapendekezo ya
kikao cha makatibu wakuu wa wizara za sekta ya kilimo kilichofanyika tarehe 30
Agosti 2018 pia kujadili namna bora ya Uratibu wa ASDP II, na Mikakati ya
kutafuta fedha za kugharamia utekelezaji wa ASDP II.
Katika Mkutano huo Mwenyekiti ambaye ni Waziri wa Sera,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na walemavu Mhe Jenista Mhagama (Mb) aliitaka timu
ya ASDP II Taifa kueleza kwa kina mikakati ya kuboresha masoko ya mazao ya
kipaumbele yaliyoainishwa katika utekelezaji wa ASDP awamu ya pili.
Alisema kuwa kumekuwa na uhamasishaji mkubwa kwa wananchi
kujitokeza kwa wingi kulima pindi unapofika msimu wa kilimo lakini bado hamasa
ya kutafuta masoko ni ndogo jambo ambalo linageuka karaha kwa wakulima nchi
hivyo muarobaini wa kutafuta masoko ndio njia pekee ya kumkomboa mkulima.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba
akizungumza katika kikao hicho alisema kuwa “ Majira ya Nchi yetu tunaendeshwa
na msimu wa kilimo hivyo tunapaswa kutekeleza mpango wa kuendeleza sekta ya
kilimo kwa haraka ili kuendana na msimu” Alisema.
Aidha, alisema kuwa punde utekelezaji utakapoanza wafadhili
wa mradi huo wanapaswa kupewa uhuru wa kuchagua eneo watakalosaidia ili
kuongeza chachu na ufanisi wa haraka katika uwajibikaji.
Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji
amewahakikishia mawaziri hao wa sekta za kilimo kuwa, wizara yake imejipanga
vyema katika utekelezaji wa Mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili
(ASDP II).
“ Wengi wamezoea kuiita wizara yetu kama wizara ya madeni
sasa tumejipanga vyema katika utekelezaji wa ASDP II kwani tunaamini kabisa
kuwa ili kuwa na uchumi mzuri ulioimarika kwa wananchi na Taifa kwa ujumla
tunahitaji kuwa na kilimo madhubuti “ Alikaririwa Dkt Kijaji
ASDP II inalenga katika mnyororo wa thamani wa mazao ya
kipaumbele na ikolojia ya kanda ya kilimo tofauti na utekelezaji wa ASDP awamu
ya kwanza ambao ulifanyika nchi nzima na kuwa na miradi karibu sekta ndogo zote
za serikali na vipaumbele na maamuzi ya uwekezaji wa Mamlaka za serikali za
mitaa.
Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa ASDP II Mazao ya
kipaumbele yaliyochaguliwa kwa kilimo ni Mchele, Mahindi, Mtama/Uwele, Muhogo,
Mboga/Matunda, Mazao ya Mbegu za mafuta (Alizeti, Ufuta, Nazi, Michikichi n.k)
Pamba, Kahawa, Sukari, Korosho, Chai, Viazi mviringo na vitamu, Mikunde, Ndizi,
na kwa Mifugo na Uvuvi ni Maziwa, Nyama (Ng’ombe), Mbuzi na Kondoo, Kuku,
samaki na Mwani.
Malengo ya ASDP II ni kuleta mageuzi ya sekta ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi ili kuongeza uzalishaji na tija, kufanya kilimo kiwe cha
kibiashara zaidi na kuongeza pato la wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha
maisha yao, usalama wa chakula na lishe.
No comments: