Naibu Waziri Nyongo ambana Mwekezaji kuhusu mpango wa huduma kwa jamii
Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.
Na Greyson Mwase, Dodoma
Naibu Waziri
wa Madini, Stanslaus Nyongo ametoa siku mbili kwa kampuni inayojishughulisha na
uchimbaji wa madini ya vito katika Kijiji cha Kwahemu wilayani Chamwino mkoani
Dodoma ya Ruvu Gemstone Mining Co. Limited inayomilikiwa na Kimon Dimitri
kuwasilisha ofisini kwake ripoti ya utekelezaji wa mpango wa utoaji wa huduma
kwa jamii kwa kipindi cha miaka miwili
kabla ya kutoa maamuzi ya serikali.
Naibu Waziri
Nyongo aliyasema hayo jana tarehe 06 Oktoba, 2018 alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kwahemu kilichopo Wilayani
Chamwino mkoani Dodoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku moja katika Wilaya ya Chamwino yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji
wa madini, kusikiliza na kutatua kero za
wachimbaji wa madini pamoja na wananchi wanaozunguka migodi.
Katika ziara
yake Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya
ya Chamwino, Vumilia Nyamoga, Mbunge wa Jimbo la Chinolwa, Joel Makanyaga, Kaimu Afisa Madini
Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Joshua Nduche, vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya pamoja na
waandishi wa habari.
Alisema
kuwa, haiwezekani kampuni inayoendesha shughuli za uchimbaji wa madini ya vito
ya Ruvu Gemstone Mining Co. Limited ikaendesha shughuli zake pasipo kunufaisha
wananchi wanaozunguka migodi yake.
Aliendelea
kusema kuwa, Serikali kamwe haitamvumilia mwekezaji wa aina yoyote
atakayeendesha shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini kwa kukiuka Sheria Mpya ya Madini yenye kipengele kinachowataka wawekezaji
kuchangia katika uboreshaji wa huduma za jamii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
vituo vya afya, miundombinu ya barabara na shule.
“Serikali
kupitia Wizara ya Madini imejipanga katika kuhakikisha watanzania wote
wananufaika na uwepo wa rasilimali za madini kupitia kodi, tozo mbalimbali
pamoja na mpango wa utoaji wa huduma za jamii,” alisema Naibu Waziri Nyongo.
Alisisitiza
kuwa, ni lazima nakala za ripoti zisambazwe kwa Mwenyekiti wa Kijiji, Diwani na
Mbunge ili kubaini ukweli wa madai ya
mwekezaji kuwa amekuwa akichangia katika huduma za jamii tangu alipoanza
kuchimba madini ya vito mwaka 1986.
Katika hatua
nyingine, Naibu Waziri Nyongo alimtaka mwekezaji kuhakikisha anadumisha mahusiano na jamii
inayozunguka mgodi ili kuepusha migogoro
inayotokea mara kwa mara.
Awali
wakiwasilisha kero kwa Naibu Waziri Nyongo wananchi wa kijiji hicho walimweleza
kuwa tangu kuanzishwa kwa mgodi husika hawajaona manufaa ya aina yoyote zaidi
ya kunyanyaswa kwa kunyang’anywa ardhi, kupigwa na wakati mwingine kufungwa
jela.
Akiwasilisha
kero kwa niaba ya wananchi hao, Daudi Kiloka ambaye ni mkazi wa kijiji cha
Kwahemu alisema kuwa awali walikuwa na shamba kubwa lenye ukubwa wa takribani
heka 500 chini ya Umoja wa Bega kwa Bega
wa kijiji hicho lakini baadaye shamba hilo lilikuja kutwaliwa na mwekezaji
huyo.
Aliendelea
kusema kuwa, wananchi wamekuwa wakikosa huduma muhimu ikiwa ni pamoja na shule,
maji na vituo vya afya hali inayolazimu
wananchi wengi kutumia muda mwingi kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kufuata
huduma.
No comments: