Serikali ipo tayari kusaidia wawekezaji wa madini- Nyongo
Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akibadilishana mawazo na Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa (kulia) kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kabla ya kuanza ziara ya siku moja katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ( wa kwanza mbele) akiendelea na ziara katika mgodi wa makaa ya mawe wa Edenville International (T) Limited uliopo katika kijiji cha Nkomolo II Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.
Meneja wa mgodi wa makaa ya mawe wa Edenville International (T) Limited, Jamhuri Mbamba (kushoto) akimwonesha Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) moja ya makaa ya mawe kwenye mgodi huo.
Meneja wa mgodi wa makaa ya mawe wa Edenville International (T) Limited, Jamhuri Mbamba (katikati) akielezea hali ya uzalishaji wa makaa ya mawe katika mgodi huo kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) katika ziara hiyo.
Na Greysona Mwase
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema kuwa
Serikali kupitia Wizara ya Madini ipo tayari kuwasaidia wawekezaji kwenye
shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini ili uchimbaji wao ulete manufaa
kwa nchi.
Aliyasema jana baada ya kumaliza ziara yake katika mgodi wa
makaa ya mawe wa Edenville International
(T) Limited uliopo katika kijiji cha
Nkomolo II Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku
moja katika mkoa huo yenye lengo la
kukagua shughuli za uchimbaji wa madini,
kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Katika ziara yake Nyongo aliambatana na Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi,
Mhandisi Giliard Luyoka, Katibu Tawala Msaidizi- Sehemu ya Miundombinu katika
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,
Happiness Shayo, Wataalam wa Madini, Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja
na waandishi wa habari.
Alisema kuwa katika kuhakikisha watafiti na wachimbaji wa
madini wanafanya kazi katika mazingira mazuri, Wizara ya Madini kupitia Tume ya
Madini imeanza kusogeza huduma zake kwa kuhakikisha kuwa inaanzisha ofisi za
maafisa madini wakazi katika mikoa yote ambapo mkoa wa Rukwa unatarajiwa kupata
ofisi kwa mara ya kwanza.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Nyongo aliushauri uongozi
wa mgodi huo kujikita kwenye uzalishaji wa makaa ya mawe ambayo ni bora na
kuuza katika nchi za jirani kwa kuwa mahitaji ya makaa ya mawe ni makubwa.
Aliwataka maafisa madini wakazi wa mikoa yote nchini
kuhakikisha wanashirikiana na ofisi za wakuu wa wilaya, vyombo vya ulinzi na
usalama pamoja na wawakilishi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika
zoezi la usimamizi wa upakiaji wa madini kabla ya kusafirishwa ili kudhibiti
mianya ya utoroshwaji wa madini mbalimbali.
Wakati huohuo Naibu Waziri Nyongo aliwataka wachimbaji wa
madini nchini kufuata kanuni na sheria za madini katika kuhakikisha kuwa
wanalipa kodi stahiki serikalini ili fedha ziweze kuwanufaisha wananchi kupitia
uboreshwaji wa huduma za jamii.
Awali akielezea hali ya uzalishaji wa makaa ya mawe katika
mgodi wa makaa ya mawe wa Edenville International (T) Limited, meneja wa mgodi
huo Jamhuri Mbamba alisema kuwa,
uzalishaji unazingatia mahitaji ya soko na kusisitiza kuwa kwa sasa
mahitaji ni takribani tani 3000 kwa mwezi na kuendelea kusema kuwa mgodi
unatarajia kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 15,000 za makaa ya mawe kwa
mwezi.
Aliendelea kusema kuwa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi
Oktoba 2018 jumla ya tani takribani 9941.78 za makaa ya mawe yalioshwa na
kuuzwa kwa wateja wa ndani na nje ya nchi.
Akielezea changamoto za mradi Mbamba alisema kuwa, awali
lengo kuu la mradi lilikuwa ni uzalishwaji wa umeme lakini mchakato wake
umekuwa ukichukua muda mrefu pasipo mafanikio.
Alisema hadi sasa maongezi kati ya kampuni na Serikali
kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) yamekuwa yakiendelea kwa kipindi
kirefu na kwa sasa kampuni inaandaa zabuni kama ilivyoainishwa hapo awali.
Aliongeza kuwa pia mradi ulilenga ujenzi wa njia ya umeme ya
Mbeya hadi Kigoma hadi Nyakanazi ambao haujaanza kujengwa.
No comments: