LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wajasiriamali Mwanza watakiwa kutumia vyema fursa zinazowazunguka

Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.


Judith Ferdinand, BMG
Wajasiriamali  wamehimizwa kutumia vyema fursa zinazojitokeza ikiwemo mradi wa kuwasaidia na kuwaendeleza wajasiriamali Tanzania(TLED) pamoja na kuweka mazingira bora katika kuendeleza biashara zao.

Wito huo umetolewa na Afisa Biashara Mkoa  wa Mwanza,  Anthony  Yessaya wakati akizungumza  katika sherehe ya maadhimisho ya miaka 60 nchini ya shirika la Voluntary Service Overseas (VSO)  linalosimamia mradi wa TLED, yaliyofanyika Jijini Mwanza na kukutanisha wanufaika wa mradi huo kutoka Mwanza  na Shinyanga.

Alisema hata kama mradi utaisha wajasiriamali hao wanatakiwa kuwa na kitu cha kujivunia ambacho kitakuwa kumbukumbu katika maendeleo ya biashara zao hivyo watumie fursa hiyo na nyingine zinazopatikana vizuri.

Yessaya alieleza kwamba katika mkoa wa Mwanza, mradi wa TLED umekuwa na manufaa kwa wajasiriamali kwani wameweza kukutanishwa na taasisi za kifedha ambazo zinawasaidia kuwapa mkopo kwa ajili ya kuendeleza biashara zao, elimu ya utunzaji fedha na kumbukumbu, soko pamoja na kuwakutanisha na mamlaka za udhibiti ubora wa bidhaa kama TFDA na TBS.

Alisema ili mradi utoke kwa shirika na kwenda wa wananchi ambao ndio walengwa uongozi wa VSO unatakiwa kushirikisha wadau mbalimbali  ili wachangie mawazo yao ambayo yatasaidia katika kuboresha na kufikia malengo pale wanapofanya tathimini ya mradi.

Pia alisema mradi unamanufaa makubwa kwa wajasiriamali hivyo ni fursa ya viongozi wa Chemba ya Wafanyabiashara,Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) na Chemba ya Wanawake  Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) kuwahimiza wanachama wao.

Justas alisema katika kuwasaidia wajasiriamali kwa kushirikiana na Chemba ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania(TCCIA), Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) wamekua wakifanya kazi kwa ukaribu, ambapo kupitia SIDO wajasiriamali wanaweza kupata kibali cha biashara kutoka TBS na TFDA ili kupata bidhaa zenye viwango na kuwekeza kwenye viwanda  kama serikali inavyotaka.

"Mradi unatoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo kuhusu   biashara, kuuza, usimamizi wa fedha pamoja na teknolojia, huku lengo likiwa ni kuboresha ujuzi kuhusu fursa katika masuala ya masoko, jinsi ya kufanya bishara na elimu ya ufundi sambamba na kuongeza uelewa wa wanawake kwenye kuanzisha na kukuza biashara ndogo ambazo ni endelevu," alisema Justas.

Pia alisema, waliweza kuwaleta wajasiriamali 20, 10 wakitokea Mwanza na wengine Shinyanga katika maonesho ya biashara Afrika Mashariki yaliyofanyika septemba ikiwa ni fursa ya kupata masoko, hivyo faida ilionekana baada ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt.Charles Mwijage alipotembelea banda lao aliiagiza TBS kusajili bidhaa za wajasiriamali wawili ambao wako chini ya TLED.

Hata hivyo alisema katika mradi huo, wana Mfuko wa Ufumbuzi wa  Teknolojia (Technological Innovation Fund)  ambao ni kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali mashine kwa ajili ya shughuli za uzalishaji bidhaa kwa wingi na bora kama lilivyo lengo la Serikali la kuwa na viwanda. 

Awamu ya kwanza wamewapatia mashine jumla wajasiriamali 13 mbao  sita kutoka mkoani  Mwanza  huku saba wakiwa wa  Shinyanga, kwa sasa watu wamejaza fomu kwa ajili ya maombi ya awamu ya pili  na wanatarajia wataongezeka.

Kwa upande wake Meneja  Mradi wa Kuwawezesha Vijana Kanda ya Ziwa wa VSO, Haidari Mfinanga alisema shirika hilo limekuwa likishughulika katika miradi ya kijamii nchini kama elimu, afya huku mikoa ya Mwanza na Shinyanga limejikita katika mradi wa kujikimu wa TLED  ambao umewezesha wajasiriamali katika nyanja mbalimbali  ikiwemo soko, utoaji wa msaada wa mashine kwa ajili ya kuongeza tija katika uzalishaji wa bidhaa, elimu ya biashara na utunzaji kumbukumbu pamoja na misaada ya kifedha.

Naye Mwenyekiti wa TWCC Mkoa wa Shinyanga, Joyce Egina alisema TLED inatakiwa kutoa mafunzo kwa vitendo ili kuzalisha watu wengi na wajasiriamali waweze kukopesheka wenyewe pamoja na kuwapa wanawake   elimu ya kujitambua na kujiamini kwani wengi wao wanakopa pesa kutoka vikundi mbalimbali  na kushindwa kuendeleza biashara na matokeo yake kufirisiwa.

Hata hivyo mmoja wa wajasiriamali waliohudhuria sherehe hiyo, Herman Bundala aliliomba shirika hilo kuboresha mfumo katika utoaji msaada wa mashine kwani wengi wanazihitaji katika kuongeza ufanisi wa uzalishaji pamoja na waangalie namna ya kuwawezesha ili wajifunze kwa vitendo.

No comments:

Powered by Blogger.