LIVE STREAM ADS

Header Ads

Maonesho ya bidhaa za vijana yafana Jijini Mwanza


Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula (katikati kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Godfrey George (kushoto) ambaye ni mtengeneza majiko akiwa ni miongoni mwa wanufaika wa mradi wa vijana kutoka Shirika la SOS Village Children's Tanzania katika maonesho ya bidhaa zinazozalishwa na vijana waliowezeshwa na shirika hilo.
Mwenyekiti wa kundi la The Forest, Elvis Felix (wa pili kulia) linalojishughulisha na utengenezaji wa batiki na sabuni za maji akitoa ufafanuzi kwa Mbunge Mabula.
Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Stanslaus Mabula (wa kwanza kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa kikundi cha Vijana Kazi Kwanza, Baraka Donald (wa kwanza kulia) kinachotengeneza sabuni za mche kutoka Kata ya Igogo ambao ni wanufaika wa mradi wa vijana kutoka Shirika la SOS Village Children's Tanzania
Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula (kushoto) akiangalia nyumba ya boksi iliyobuniwa na vijana ambao ni wanufaika wa mradi wa vijana kutoka Shirika la SOS Village Children's Tanzania
Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula akizungumza katika maonesho ya vijana wanaofaika na mradi wa Shirika la SOS Village Children's Tanzania.


Judith Ferdinand, BMG
Katika kuhakikisha vijana wa Wilaya ya Nyamagana wanafanya shughuli za kiuchumi na kuacha kuwa tegemezi sambamba na kusaidia familia zao, Shirika la SOS Villages Children's Tanzania limewawezesha jumla ya vijana 175 katika nyanja mbalimbali.

Akizungumza na BMG baada ya kumalizika kwa maonesho ya bidhaa zinazozalishwa na vijana hao yaliyofanyika Jijini Mwanza, Mratibu wa Maendeleo ya Jamii wa Shirika la SOS Village Children's Tanzania Mkoa wa Mwanza,  Samson Anthony alisema mradi wa kuwainua vijana ulioanza 2018 hadi 2020 una lengo la kuwasaidia vijana kuweza kujitegemea kwa kuwakutanisha na taasisi ambazo zitawapatia ujuzi mbalimbali ambapo kwa kipindi hiki cha mradi wana jumla ya vijana 175.

Anthony alisema kati ya vijana hao, tayari vijana 45 wamehitimu mafunzo ya ushonaji wa nguo kutoka VETA huku wengine wakipatiwa mafunzo ya ujasiriamali kutoka SIDO ambapo wamejifunza utengenezaji wa karanga za mayai, batiki, dawa za chooni, dawa za kusafishia vigae, sabuni za miche na maji huku wengine wakipatiwa mitaji kwa ajili ya kuanzisha biashara ikiwemo kilimo cha mbogamboga, utegenezaji wa majiko, upambaji, ufundi wa vifaa vya umeme, wabunifu, uuzaji wa juisi na matunda, uuzaji wa nafaka, ususi pamoja na kinyozi.

Alisema baada ya kupatiwa mafunzo vijana hao wameanza shughuli rasmi za uzalishaji mali na kuingia sokoni ambapo katika maonesho hayo wameshuhudia bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa kwa ubora, hivyo wataweze kusaidi familia zao pamoja na watoto ambao shirika ndio imewalenga zaidi,kuacha kuwa tegemezi na kujitegemea kiuchumi sanjari na kutokuwa na muda wa kufanya masuala ya uhalifu ikiwemo utumiaji wa dawa za kulevya,wizi hivyo kujiletea maendeleo binafsi, wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla na hatimaye kuajiri wengine, imesaidia Serikali kutatua changamoto ya ajira.

Pia alisema kwa sasa mradi unafanya kazi katika kata tano za wilaya ya Nyamagana ikiwemo Mkuyuni, Mahina, Igogo, Pamba, Mandu na Kata ya Bugogwa iliopo wilayani Ilemela ambapo vijana wamepatiwa elimu ya utunzaji kumbukumbu na fedha.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Stanslaus Mabula aliyekuwa mgeni rasmi katika maonesho hayo alilipongeza shirika hilo, kuwasaidia vijana kwa kuwapatia ujuzi mbalimbali, mitaji na kuwaunganisha na halmashauri kwani wameweza kutengeneza na kuzalisha bidhaa kama batiki, hivyo kuweza kuanzisha viwada vidogo kama Serikali inavyotaka atahakikisha fedha za mfuko wa vijana zinawafikia ili waweze kujiendeleza zaidi kwani awali walikua wanashindwa wazipeleke wapi kutokana na vijana wengi kushindwa kurehesha mkopo.

Naye Mwenyekiti wa Vijana wa Shirika hilo Yusuph Ng'ahala alisema shirika limewasaidia mitaji,ujuzi ili vijana kufanya biashara pamoja na kuwaunganisha na ajira moja kwa moja kwa wale wenye elimu, na wanakutana mara mbili kwa mwezi ili kukumbushana na kujadili changamoto wanazokutana nazo pamoja na kuzipatia ufumbuzi ili wasiweze kurudi nyuma pia vijana wanatakiwa kuwa wavumilivu katika kujiletea maendeleo.

Mmoja wa wanafaika wa mafunzo ya ushonaji wa nguo, Dora Daniel alisema vijana wajitokeze wanaposikia fursa kama hizo kwani ni njia pekee ya kujiendeleza kimaisha na wasidharau kwani ukiwa na ujuzi utaweza kujitegemea wenyewe ila kwa sasa wanaupungufu wa cherehani za kawaida, ukosefu wa cherehani ya overlocks na ya kudarizi.

No comments:

Powered by Blogger.