LIVE STREAM ADS

Header Ads

TCRA yawapiga msasa mafundi simu Jijini Mwanza kabla ya kuanza kuwasajili

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Judith Ferdinand, BMG
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka mafundi simu mkoani Mwanza kujaza taarifa sahihi na za kweli katika fomu ambazo zitawasaidia kutambulika na kupatiwa cheti cha usajili.

Kauli hiyo ilitolewa na Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Francis Mihayo katika semina ya kuwaelimisha mafundi hao kuhusu tangazo lililotolewa na mamlaka hiyo linalowataka wajisajili ili watambulike kisheria na kuongeza kwamba katika zoezi hilo fomu na usajili ni bure hivyo ni muhimu wahusika kujaza taarifa ambazo ni sahihi na za kweli.

"Tumekubaliana baada ya wiki moja wote muwe mmechukua fomu na kujaza taarifa sahihi ikiwemo majina kamili, kiwango cha elimu, anuani ya makazi, namba ya simu na kurudisha fomu huku mkiambatanisha kitambulisho cha mpiga kura, uraia au leseni ambapo kwa Mkoa wa Mwanza tuna nakala 300 ambazo tutawapatiwa viongozi wenu ili iwe rahisi kuzipata na kila mmoja atapatiwa cheti huku nakala zikipelekwa polisi ili kusaidia wakati wa zoezi la ukaguzi". Alisema Mihayo.

Alisema lengo la usajili huo ni kuwasaidia mafundi hao kufanya shughuli zao kwa kufuata utaratibu kwani kumekuwepo na malalamiko katika utengenezaji wa simu na wengi wamekuwa wakijikuta wanaangukia kwenye mtego wa kubadilisha IMEI kwenye simu zilizoibiwa.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Mafundi Simu Mkoa wa Mwanza,  Maguwa Manyanda aliipongeza Serikali kupitia TCRA kwa hatua hiyo ya kuwatambua hivyo na taasisi zingine ziige mfano huo na kuwasaidia pale wanapotaka msaada kwani wamekuwa wakichukuliwa kama wahuni na wezi lakini kupitia wao wanaweza kusaidia jamii kupata simu zilizoibiwa kwani mteja akihitaji kutengeneza simu sasa lazima aombwe kitambulisho chake.

Alisema wanachoomba ni ushirikiano kwani umoja huo una wanachama zaidi ya 200 na kila mmoja lazima ajaze fomu hivyo wao kama viongozi hawatatoa fomu kwa mtu ambaye si fundi simu.

No comments:

Powered by Blogger.