LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wadau wajadili rasimu ya kanuni za uanzishwaji masoko ya madini Tanzania

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Katibu Mkuu wa Madini, Prof Simom Msanjila mbele (mwenye koti jeusi) akiongoza kikao cha kupokea maoni juu ya rasimu ya uanzishwaji wa kanuni za masoko ya madini nchini.
Katibu Mkuu wa Madini, Prof. Simon Msanjila akifafanua jambo wakati wa upokeaji wa maoni kutoka kwa wawakilishi wa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini juu ya rasimu ya uanzishwaji wa kanuni za masoko ya madini nchini.
Washiriki wa kikao cha kutoa na kupokea maoni juu ya rasimu ya uanzishwaji wa kanuni za masoko ya madini nchini wakisubiri kuanza rasmi kwa kikao hicho.
Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa Wizara, Edwin Igenge akiwasilisha rasimu ya kanuni za uanzishwaji wa masoko ya madini nchini.
Wajumbe wa mkutano wa kutoa na kupokea maoni juu ya rasimu ya uanzishwaji wa kanuni za masoko ya madini nchini wakifuatilia mada.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila (wa sita kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa wachimbaji wadogo wa madini waliofika ili kutoa maoni yao juu ya rasimu ya kanuni za uanzishwaji wa masoko ya madini nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila (wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa wachimbaji wadogo wa madini waliofika ili kutoa maoni yao juu ya rasimu ya kanuni za uanzishwaji wa masoko ya madini nchini. Kulia kwa Katibu Mkuu ni Rais wa FEMATA John Bina na Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa Wizara Edwin Igenge.

Na Nuru Ikupa, Wizara Madini
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila ameongoza kikao kilicholenga kupokea maoni juu rasimu ya kanuni za uanzishwaji wa masoko ya madini nchini.

Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa wizara kimewakutanisha, Makamishna Wasaidizi wa Wizara, Rais wa Shirikisho la Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) John Bina, viongozi wa shirikisho hilo pamoja na wawakilishi wa wachimbaji wadogo kutoka mikoa ya kimadini nchini.

Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa kikao, Prof. Msanjila alisema maoni ya wajumbe hao ni muhimu kwa watanzania na taifa kwa ujumla katika kuboresha kanuni hizo.

Aidha, Msanjila amebainisha kuwa, wadau wengine wamekwisha kutoa maoni yao katika makundi tofauti tofauti na pia maoni mengine yanaendelea kupokelewa kwa njia ya maandishi na kuwataka maoni hayo yakamilishwe ndani ya kipindi cha wiki moja.

Kabla ya kupokea maoni hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa Wizara, Edwin Igenge aliwasilisha rasimu ya kanuni hizo ili kutoa uelewa wa kile wanachopaswa kuchangia katika kutoa maoni yao.

Akiwasilisha rasimu hiyo, Igenge alisema hii ni sheria ndogo inayotokana na sheria mama ya madini. “Kanuni hizo zinatungwa kwa mujibu wa kifungu cha 27 (C) kifungu kidogo cha pili pamoja na kifungu cha 129 cha sheria ya madini,” amesema Igenge.

Aidha, amesema mahala patakapo kuwa na soko la madini kutakuwa na huduma zote zinazotakiwa ili kurahisisha ubadilishwaji wa fedha na madini kama vile mabenki, ofisi za mamlaka ya Mapato (TRA), ofisi za masuala ya ulinzi na usalama, pamoja na ofisi mbalimbali za serikali.

Igenge amesema baada ya kukamilika na kupitishwa kwa kanuni hizo zitatafsiriwa na kupatikana katika lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi wote kuelewa kanuni na mwongozo wa masoko ya madini.

Akizungumzia baadhi ya vipengele vilivyopo katika rasimu hiyo, Igenge alisema sehemu ya kwanza inahusika na utangulizi yenye vifungu 3 cha kwanza ni jina la kanuni ambapo litaitwa ‘Kanuni za masoko za mwaka 2019’, pili ni maelezo ya wapi kanuni hizo zitatumika na kuratibiwa na kipengele cha mwisho kitatoa tafsiri ya maneno mbalimbali yanayotumika ndani ya kanuni hizo.

Sehemu ya pili ya kanuni inahusika na uanzishwaji wa masoko yenyewe, ambapo masoko yataanzishwa katika maeneo yenye tawala za mikoa na kuipa maelekezo Tume ya Madini kuhakikisha wanashirikiana na tawala za mikoa katika kuanzisha masoko hayo.

Aidha, alielezea msingi wa kwanza ni msingi wa uwazi, msingi wa matangazo ili watu waweze kujua madini yanauzwa na kununuliwa wapi, msingi wa haki ambao utazuia manunuzi haramu ya madini, lakini pia msingi wa mwendelezo ikiwa na maana masoko hayo kuwa ni masoko ya kudumu na si ya msimu.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, ameiomba serikali kuyafanyia kazi maoni yaliyotolewa na wawakilishi wa wachimbaji wadogo ili kupata kitu kitakachokubalika na jamii nzima ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini.

Aidha, alikiri kufurahishwa na ufafanuzi uliotolewa katika kila kipengele cha rasimu ya kanuni za uanzishwaji wa masoko ya madini na kukiri kwamba wanaamini kuwa serikali ina nia njema na wananchi wake.
#PamojaDaimaBMG

No comments:

Powered by Blogger.