Majukwaa ya NAWEZA na SITETEREKI kuzinduliwa Kanda ya Ziwa
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Judith Ferdinand, BMG
Serikali kupitia
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imejipanga kuboresha
huduma za afya ya uzazi kwa akinamama, watoto chini ya umri wa miaka mitano
pamoja na vijana kupita majukwaa ya Naweza na Sitetereki chini ya mradi wa Tulonge
Afya unaofadhiliwa na shirika la watu wa Marekani (USAID).
Akizungumza jana
na waandishi wa habari jijini Mwanza, Afisa Mradi wa Afya ya Uzazi Salama (MOHCDGEC)
kutoka wizara hiyo, Martha Shakinyau alisema majukwaa hayo yanalenga kutoa elimu kwa umma ili kupunguza
vifo vya akina mama wakati wa kujifungua kutoka vifo 556 kati ya vizazi hai 100,000
kwa mwaka hadi kufikia 292 ifikapo mwaka 2020.
Alisema pia yamelenga kuwahamasisha akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki
kwani idadi ya wanaohudhuria klinikini hivi sasa ni asilimia 25 huku malengo
yakiwa ni kuongeza idadi hiyo hadi kufikia asilimia 70 mwaka 2020.
Aidha
alibainisha kwamba asilimia 63 ya akina mama wajawazito ndio hujifungulia
katika Vituo vya Afya ama Hospitalini huku asilimia 34 wakifika kwenye huduma
za afya baada ya kujifungua.
“Tumekuja na
jukwaa la Naweza ili baba, mama, familia na kila mmojkatika jamii aweze kuwajibika
katika kuwashawishi na kuelimisha akinamama wajawazito kwenda kliniki pale wanapogundua
kuwa na ujauzito”. Aalisema Shakinyau.
Naye Afia Mradi
wa Mawasiliano ya Afya, Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya
Afya, Dkt. Tumaini Haonga alisema waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya
kusaidia akinamama na jamii kwa ujumla kupata elimu ya uzazi ili kufikia
asilimia 70 ya wajawazito wanaohudhuria kliniki kabla na baada ya kujifungua.
Kwa upande
wake Mratibu wa Afya ya Uzazi kwa Vijana kupitia jukwaa la Sitetereki, Gerald
Kihwele alisema jukwaa hilo limeanzishwa kwa lengo la kuboresha shughuli za
mawasiliano ya mabadiliko ya tabia kwa vijana kuanzia miaka 15 hadi 24 nchini
na kuwahamasisha kuwa na tabia za kiafya ambazo zitaboresha hali zao na afya
kwa ujumla.
Mkurugenzi wa Mawasiliano, Mradi USAID Tulonge Afya, Prisca
Rwezahura alisema waandishi wa habari wanategemewa katika kuboresha huduma za afya
kwa kutoa elimu kwa wananchi ili kubadilika na kulinda afya zao.
Majukwaa ya NAWEZA na SITETEREKI kupitia mradi wa Mradi wa
Tulonge Afya yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi Machi 06 na 07, 2019 kwa mikoa ya
Kanda ya Ziwa ambapo uzinduzi huo unafanyika Jijini Mwanza. Tazama BMG Online TV hapa chini
No comments: