LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wanawake Wizara za Madini na Nishati waadhimisha "Siku ya Wanawake Duniani"

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Wawakilishi wa wanawake kutoka Wizara za Madini, Nishati na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) wakiwa njiani kuelekea katika vituo vya watu wenye mahitaji maalumu katika Kata ya Buigiri, Halmashauri ya Chamwino, Jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 08.
Wanawake Watumishi wa Wizara za Nishati na Madini katika picha ya pamoja walipojumuika na watu wenye mahitaji maalumu ikiwa ni moja kati ya matukio katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Mwakilishi wa wanawake watumishi waliojumuika katika kutoa misaada kwa watoto na watu wazima wenye mahitaji maalum Remida Ibrahim (kushoto) akieleza lengo la ziara hiyo kwa Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya walemavu wasioona Mwalimu Historia Mputa (Kulia) ofisini kwake.
Wawakilishi wa wanawake kutoka Wizara za Madini, Nishati na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) wakiongozwa kuelekea eneo maalum tayari kwa ajili ya kukutana na wanafunzi wasioona pamoja na kupata historia fupi ya shule hiyo.
Mwakilishi wa Wanawake waliojumuika katika kutoa misaada kwa watoto na watu wazima wenye mahitaji maalum Remida Ibrahim (kushoto) akizungumza na watoto wenye ulemavu waliokusanyika ili kuitikia mwito huo.
Wawakilishi wa wanawake kutoka Wizara za Madini, Nishati na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) (katikati) wakikabidhi zawadi kwa mmoja wa watoto wenye ulemavu (Kulia) na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo (kushoto) Historia Mputa.
Wawakilishi wa wanawake kutoka Wizara za Madini, Nishati na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi na baadhi ya watumishi wa shule ya wenye walemavu wa kuona mara baada ya kuhitimisha zoezi lililowapeleka kituoni hapo.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya walemavu wasioona (wa pili kutoka kushoto mbele) Historia Mputa akitoa shukrani kwa wanawake waliofika kutoa salamu kwa ajili ya kusheherekea Maadhimisho ya Siku ya wanawake katika Kata ya Buigiri, Halmashauri ya Chamwino Mkoani Dodoma.
Mwenyekiti Msaidizi wa kituo cha watu wazima wasioona, Yusuph Matando akiukaribisha ujumbe wa wawakilishi wanawake kutoka Wizara za Madini, Nishati na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) waliotembelea katika kituo hicho.
Mwakilishi wa Wanawake waliojumuika katika kutoa misaada kwa watoto na watu wazima wenye mahitaji maalum Juntwa Mwakahesya aliyewakilisha Wizara ya Nishati akieleza lengo la kutembelea katika kituo chao.
Kushoto ni Angelister Sylivester mjumbe kutoka GST na kulia Cecilia Mlope wakikabidhi zawadi kwa watu wenye ulemavu wa kuona baada ya kuwatembelea katika kituo chao.
Wawakilishi wa wanawake kutoka Wizara za Madini, Nishati na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) wakiwa katika picha ya pamoja na watu wazima wenye ulemavu wa macho walipowatembelea katika kituo chao kilichopo Kata ya Buigiri Halmashauri ya Chamwino, Jijini Dodoma.

Na Nuru Mwasampeta, Dodoma
Katika kuelekea Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Wanawake kutoka Wizara za Madini, Nishati na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), jana wamefanya Matendo ya Huruma kwa kuwatembelea watu wenye mahitaji maalum na kutoa mahitaji mbalimbali ya kijamii.

Vituo vilivyotembelewa na wanawake hao ni Shule ya watoto wasioona na kituo cha watu wazima wasioona vilivyopo katika Kata ya Buigiri, Halmashauri ya Chamwino jijini Dodoma kwa lengo la kujumuika pamoja kabla ya kilele cha maadhimisho hayo ambayo hufanyika tarehe 8 Machi, kila mwaka.

Akizungumza kwa niaba ya ujumbe huo mara baada ya kuwasili katika shule ya watoto wasioona, Afisa Utumishi kutoka Wizara ya Madini anayeshughulikia masuala ya wanawake Remida Ibrahim, amesema kutokana na wanawake kuguswa zaidi na masuala ya kijamii ndio sababu iliyopekea ujumbe huo kufika kituoni hapo kwa ajili ya kutoa mahitaji mbalimbali ili yaweze kuwasaidia watoto hao.

Remida amewaasa wanafunzi hao ambao asilimia tisini na tano wana ulemavu wa kutokuona kusoma kwa bidii ili kujikwamua na maisha yao ya baadaye na kuwataka kuelewa kuwa Serikali inatambua uwepo wao na kwamba iko bega kwa bega katika kuhakikisha inachangia katika kutoa elimu bora.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo, Historia Mputa, ameushukuru ujumbe wa wanawake kutoka katika makundi hayo kwa kutoa kipaumbele kwao na kuamua kutembelea kituo hicho na kueleza, “vituo vya watoto wenye mahitaji maalum ni vingi sana lakini mmeona vema kututembelea mahala hapa tunashukuru sana”, amesisitiza.

Baada ya kukamilisha shughuli ya kukabidhi zawadi katika kituo hicho, ujumbe hao ulihamia katika kituo cha wasioona watu wazima ambapo walipata fursa ya kusikia historia fupi ya kituo na kusikiliza kero mbalimbali zinazokikabili kituo hicho na baadaye kukabidhi bidhaa zitakazosaidia katika kupata mahitaji kwa siku kadhaa.

Akizungumzia uanzishwaji wa kituo hicho, Mwenyekiti Msaidizi wa kituo hicho Yusuph Matando, amesema kituo hicho kilianzishwa mnamo mwaka 1992 na Mwalimu Keneth D. Mwanampalila na kufadhiliwa na Kendall Lee wa nchini Uingereza kwa lengo la kuwasaidia watu wasioona kujipatia mahitaji yao kwa shughuli za kilimo cha mbogamboga badala ya watu hao kuombaomba mtaani.

Yusuph amebainisha changamoto zilizopo kituoni hapo kuwa ni hicho kuwa ni pamoja kutokufikiwa na huduma ya umeme ,ugumu katika upatikanaji wa mbegu, uhaba wa mipira ya maji kwa ajili ya kumwagilia bustani zao pamoja na maji yanayopatikana katika kisima hicho kutokutosheleza mahitaji ya kijiji.

Siku ya wanawake duaniani huadhimishwa tarehe 8 Machi ya kila mwaka ikilenga kusisitiza kujenga mshikamano wa wanawake wote duniani, kuelimisha kuhusu jitihada zinazofanywa na serikali na taasisi zisizo za serikali katika kuwaendeleza wanawake na kuhamasisha utekelezaji wa Sera na mipango ya Serikali yenye lengo la kudumisha amani, usawa na maendeleo.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Mwaka 2019 ni “ Badili fikra, fikiria usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu’’.

No comments:

Powered by Blogger.