LIVE STREAM ADS

Header Ads

Viongozi wanaopachika habari zao mitandaoni bila kusajiliwa waonywa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Na Kadama Malunde, Malunde 1 Blog
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema haiwezi kuzungumza chochote kuhusu gharama za usajili wa mitandao ya kijamii inayotoa maudhui ya habari mtandaoni kwa sababu ni sheria na ili kupunguza gharama hizo lazima mchakato wa kisheria ufuatwe kwa kupitia bungeni.

Kauli hiyo ilitolewa jana Machi 08, 2019 na Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Francis Mihayo wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya utangazaji kupitia Televisheni na Redio za kawaida na za mitandaoni (Blogs & Online Tv) kutoka Kanda ya Ziwa Victoria uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza.

Mhandisi Mihayo alitoa kauli hiyo akijibu swali la mmiliki wa Malunde Media (Malunde 1 blog), Kadama Malunde aliyeiomba TCRA kupunguza gharama za usajili wa Mitandao ya Kijamii (kwa sasa ada ya leseni ni shilingi Milioni Moja kwa mwaka na ada ya maombi ni shilingi Laki Moja) ili kuwasaidia vijana walioamua kujiajiri kupitia mitandaoni.

"Hizi gharama wanazotozwa hawa watoa huduma za maudhui mtandaoni ni ndogo ukilinganisha na zile gharama zinazolipwa na watu wa Televisheni na Radio, kwanza watu wa mtandaoni wana leseni ya kimataifa, anapochukua habari anaenda kuzipakia kwenye mtandao zinaonekana dunia nzima lakini ninyi (Tv na Radio) mna leseni kulingana na eneo husika". Alisema Mhandisi Mihayo na kuongeza;

"Kwa hiyo Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) hatuwezi kuzungumzia chochote kuhusu hizi gharama za usajili kwa sababu ni sheria, sisi tunatekeleza sheria, kwa hiyo hizi gharama nafikiri ukitaka zipungue ni lazima mchakato wa kisheria ufuatwe kwa sababu lazima upitie bungeni". Alieleza.

Awali akitoa taarifa ya vituo vya utangazaji wa maudhui mtandaoni Kanda ya Ziwa, Mhandisi Mihayo alisema mpaka sasa TCRA inasimamia vituo 36 vya Redio, Televisheni tatu na watoa huduma wanne wa maudhui mtandaoni waliosajiliwa kwa mujibu wa sheria ambao ni Mohab Online TV, Geita Online TV, Binagi Blog pamoja na Malunde Media.

"TCRA inaendelea na zoezi la kuwabaini watoa huduma mtandaoni ambapo mpaka sasa Kanda ya Ziwa tulishawatambua 24 na kuwatahadharisha kuacha kuvunja sheria kati yao wapo waliotii agizo la Mamlaka kwa kusitisha kwa muda upakiaji wa habari mtandaoni na wanaendelea na taratibu za usajili". Alisema na kuongeza;

"Wengine wameendelea kukaidi agizo la mamlaka na kuendelea kuvunja sheria kwa kisingizio eti wanaandika habari za viongozi mbalimbali wa mikoa na wilaya, niwakumbushe viongozi hao kuwa sheria ya usajili wa watoa huduma mtandaoni "Online Tv, Blogs, Online radio, simulcasting online Tv na Radio,Weblogs) ipo kwa ajili ya wote zikiwemo taasisi za serikali.

Mhandisi Mihayo alisema "TCRA inawashauri viongozi waache kusaidia kuvunja sheria ama kwa kujua au kwa kutojua kwa kuwatumia waandishi wanaopakia habari za matukio mbalimbali yanayowahusu kwenye mitandao ya kijamii inayotakiwa kusajiliwa, tutaendelea kuwachukulia hatua za kisheria ili kila mtoa huduma mtandaoni afanye kazi kwa kufuata sheria".

"TCRA inawafahamu watu wote wanaopakia maudhui mtandaoni hivyo wale wanaoendelea kutoa maudhui mtandaoni ni lazima wafuate taratibu za kisheria ikiwemo kujisajili, tunaendelea kuwafuatilia na watashughulikiwa na vyombo vya kisheria". Aliongeza.

"Kuna wale ambao wameamua kuhamishia kazi za blogs Instagram na Facebook, hawa nao tutawashughulikia". Alisisitiza Mhandisi Mihayo.

No comments:

Powered by Blogger.