LIVE STREAM ADS

Header Ads

Maadhimisho ya siku ya kimataifa ya "Red Cross 2019" kufanyika Kigoma

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Na Mwandishi Maalum
Tanzania Red Cross Society leo inaungana na nchi 191 ulimwenguni katika maadhimisho ya siku ya Red Cross Duniani Mei 8, 2019 ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Kigoma katika viwanja vya Mwanga Community Center kuanzia saa tatu asubuhi. Mgeni rasmi anatarajia kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako.

Katika maadhimisho hayo, Prof. Ndalichako atazindua bweni la wanafunzi katika shule ya Bitale lililojengwa kwa michango wanachama na wafanyakazi ili kuwasaidiawatoto wenye ulemavu watimize ndoto zao.

Kauli Mbiu ya mwaka huu kimataifa ni "Upendo". Ujumbe huu unamaanisha kwamba Red Cross inawafikia na kuwahudumia watu na jamii nyakati zote katika hali mbalimbali bila ubaguzi wa aina yoyote kwa upendo.

Tanzania Red Cross Society inafanya kazi kwa bidii na kutoa huduma za kibinadamu kwa kufuata kanuni zake saba za Ubinadamu, Uadilifu, Kutopendelea, Uhuru, Kujitolea, Umoja, na Kushirikiana kimataifa ambapo hii inaifanya jamii kuiamini na kuikisaidia kutimiza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Red Cross imekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma wakati wa maafa na dharura mbalimbali ikiwemo mafuriko, njaa, tetemeko, ajali mbalimbali za nchi kavu na majini, kushiriki juhudi za kuboresha afya ya jamii na kuhamasisha upatikanaji damu salama, huduma kwa watu wanaoishi na maambukizi. 

Kwa miaka zaidi ya 20 imekuwa ikitoa huduma za kibinadamu kwa wakimbizi, kwa sasa inatoa huduma za afya kwa zaidi ya wakimbizi 300,000 katika kambi za Nyarugusu (Wilaya ya Kasulu) na Mtendeli (Wilaya ya Kakonko), pia inatoa huduma za kuwaunganganisha wana ndugu waliopoteana (Restoring Family Links).

Katika maadhimisho ya mwaka huu, kupitia matawi yake ya Mikoa na Wilaya, Tanzania Red Cross imefanya shughuli za kijamii ikiwemo kusafisha mazingira, kusaidia vikundi vilivyo katika mazingira hatarishi na kuhamasisha watu uchangiaji damu kwa hiari, michezo, kambi ya vijana, kupanda miti na mafunzo kuhusu huduma za afya ikiwemo huduma ya kwanza.

Katika Wilaya ya Kasulu, kwa kushirikiana na Halmashauri husika TRCS imejenga maabara za kisasa katika vituo vya afya vitatu kikiwemo cha Rusesa katika kata ya Rusesa, Nyenge (Kurugongo) na hospitali ya Kimwanya iliyopo katika Kata ya Nyachenda.

Katika Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma TRCS kwa ushirikiano na Belgium Red Cross inaendelea kutekeleza mradi wa Maji na afya ya msingi kwa kuwasaidia wanachi kujenga vyoo vya kisasa na kujenga uzio katika vyanzo vya maji katika vijiji saba vya Buhigwe, Kavomo, Murela, Songambele, Bulimanyi, Nyamugali na Munyegera ambapo hadi sasa familia 200 wamesaidiwa vifaa na kujenga vyoo vya kisasa.

Tanzania Red cross Society inaiomba jamii kuendelea kutoa huduma za kijamii kwa kufuata maadili ya kibinadamu na kuifikia jamii popote ilipo na kila wakati.

No comments:

Powered by Blogger.