Mashindano ya UMISSETA 2019 yafikia tamati mkoani Shinyanga
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko, amefunga rasmi mashindano ya michezo kwa shule za Sekondari (UMISSETA 2019) mkoani Shinyanga na kuwataka washindi watakaoungana na kuwa timu moja ya mkoa, wakashiri kikamilifu katika mashindano hayo ngazi ya kitaifa huko Mtwara, na kupata ushindi wa makombe mengi.
Mashindano hayo ya (UMISSETA) yalifunguliwa na mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack Mei 27, 2019 ambapo yamefungwa leo Mei 30 na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, kwenye viwanja vya CCM Kambarage mjini humo, ambapo washindi wamepewa zawadi za makombe.
Mashindano yalishirikisha timu mbalimbali kutoka halmashauri ya Kahama Mji, Msalala, Ushetu, Kishapu, Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga kwa kuchezwa mpira wa miguu, kikapu, pete,tenesi, wavu, riadha, kucheza ngoma, pamoja na kuimba kwaya.
Akizungumza wakati akifunga mashindano hayo,Mboneko amewataka washiriki ambao watachaguliwa kuwa timu moja za kwenda kushiriki (UMISSETA) ngazi ya kitaifa, wawe kitu kimoja na kutobaguana kuwa huyo anatoka halmashauri nyingine, bali washindane kama timu moja ambayo inatoka mkoani Shinyanga na hatimaye kuibuka na ushindi.
“Nawapongeza wanafunzi wote mlioshiriki kwenye mashindano haya ya (UMISSETA) ambapo mmeonyesha vipaji vyenu na wote ni washindi, lakini hamtaweza wote wanafunzi 704 kwenda kushiriki ngazi ya kitaifa, bali tutachagua wanafunzi 120 ili wakatuwakilishe na tunataka mrudi na makombe mengi,” amesema Mboneko.
“Na mtakapokuwa kambini muwe timu moja na kutobaguana kuwa huyu anatoka halmashauri hii, sitaki kitu kama hicho bali nataka muwe ndugu kwani nyie wote mnatoka Shinyanga, na mkashindane kweli kweli kwa kuonyesha vipaji vyenu na kuupatia sifa mkoa wetu,”ameongeza.
Pia amewataka washindi ambao watachaguliwa kwenda kushiriki mashindano hayo ngazi ya kitaifa, wakaonyeshe nidhamu ya hali ya juu na siyo kwenda kuchafua sifa ya mkoa.
Naye Afisa Elimu mkoa wa Shinyanga Mohamed Kahundi, amewataka wanafunzi hao pindi watakapokuwa huko Mtwara, waonyeshe vipaji vyao ikiwa michezo ni ajira kwa sasa. Aidha washindi waliopatikana kwenye mashindano hayo ya (UMISSETA) Mwaka 2019 mkoani Shinyanga, mpira wa miguu wavulana ni halmashauri ya Msalala, wasichana halmashauri ya Shinyanga, mpira wa mikono (Handball) wavulana Manispaa ya Shinyanga, wasichana Kishapu, Volleyball Manispaa ya Shinyanga, wasichana halmashauri ya Shinyanga.
Kwa upande wa mpira wa kikapu wavulana na wasichana washindi ni kutoka halmashuri hya Shinyanga, mpira wa pete Kahama Mji, Tenesi mshindi wavulana na wasichana ni Halmashauri ya Shinyanga , riadha wavulana Shinyanga, wasichana Kishapu, ngoma kutoka Ushetu, kwaya Kahama Mji, usafi na nidhamu wavulana Kahama Mji, wasichana Shinyanga.
Hata hivyo katika mashindano hayo ya UMISSETA (2019) Mshindi wa jumla alitoka halmashauri ya Shinyanga , huku kauli mbiu ya mwaka huu inasema ‘MICHEZO NA SANAA KWA ELIMU BORA NA AJIRA.’
Imeandaliwa na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog
No comments: