Wizara ya Mifugo na Uvuvi yaanza kutoa mafunzo kwa wachunaji ngozi
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Na Mwandishi Maalum
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi
imeanza kutoa mafunzo ya wachunaji wa ngozi wa machinjio mbalimbali nchini ili waweze kuboresha kazi zao kwa kutoa mazao bora ya ngozi zitakazo ingiza
fedha za kigeni kutokana na mauzo ya nje na kukuza uchumi wa taifa na
kuanzishwa kwa viwanda vya ngozi.
Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko kutoka Wizara hiyo, Dkt. Felix
Nandonde ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo kwa wachunaji wa ngozi wa machinjio ya Manispaa ya Morogoro.
Dkt. Nandonde alisema Tanzania imekuwa
ikipata kiasi kidogo cha fedha za kigeni kutokana na uharibifu wa ngozi licha
ya kuwa ni nchi ya pili kwa uwingi wa mifugo Barani Afrika baada Ethiopia na
kwamba asilimia 50 ya uharibifu wa ngozi hutokea wakati wa uchunaji.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, kwa
sasa Tanzania ina ng’ombe milioni 32.2,
mbuzi milioni 20 na kondoo milioni tisa,
na kwamba ngozi zote zingeweza kusimamiwa ubora wake na kuingia katika
mfumo wa biashara ya ngozi pato la
Serikali na Wananchi lingeongezeka kwa kiwango kikubwa.
Dkt. Nandonde alisema kutokana na
mapungufu hayo, Wizara imeamua kuja na
mkakati mahususi juu ya mbinu mpya ili kuikwamua sekta ndogo ya ngozi ili na
kuifanya itoe mchango mkubwa zaidi kwa kuwapa mafunzo maalumu wachunaji wa
ngozi katika machinjio.
Hata hivyo alisema kuwa kwa sasa sekta
hiyo ya ngozi imekuwa ikitoa mchango katika pato la Serikali na mtu mmoja mmoja
ambapo kwa mwaka 2017/18 jumla ya Tsh. 5,098,846,623 zilipatikana wakati Tsh. 5,254,388,808
zilikusanywa na Serikali katika kipindi cha Machi 2018/19 kutokana na kusafirisha
ngozi na bidhaa zake nje ya nchi.
Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao
ya Mifugo, usalama wa chakula na lishe kutoka Wizara hiyo, Gabriel Bura alisema
wameamua kutoa mafunzo hayo kwa wachunaji ngozi kutokana na sheria ya biashara
ya ngozi namba 18 ya mwaka 2008 inawataka kufanya hivyo na kisha baada ya
mafunzo watapewa leseni ya uchunaji ngozi na kuweza kutambulika na Serikali.
Alisema kuwa kupitia sheria hiyo ya
ngozi mambo mengi yanatakiwa kusimamiwa ikiwemo ya machinjio yoyote wakati wa
kusajiliwa kuwepo kwa watalaam wenye mafunzo ya namna ya kuchuna ngozi na ili kuhakikisha ubora wa ngozi unasaidia
kuinua sekta ndogo ya ngozi.
Naye Afisa Mifugo Mkoa Morogoro, Dkt. Gasper
Msimbe alisema zaidi ya wachunaji wa ngozi 200 wa Manispaa ya Morogoro
watapatiwa mafunzo hayo yenye lengo la kuwapa mbinu mpya za uchunaji ili
kuhakikisha wanasaidia kupatikana kwa ngozi yenye ubora.
Mmoja wa wachunaji wa ngozi katika
machinjio hiyo ya Manispaa ya Morogoro, Alex Chiboyi alisema kupitia mafunzo
hayo yatawezesha kuzalisha ngozi yenye ubora na kuongeza kipato.
Chiboyi ambaye ana uzoefu wa miaka 20
katika uchunaji wa ngozi katika machinjio aliishukuru Serikali kwa kuanzisha
mpango huo unaoensa sambamba na utoaji wa leseni kwani zitawasaidia kuwepo na usimamizi
mzuri na kuondokana na matapeli.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya
wachunaji wa ngozi wa machinjio ya Manispaa ya Morogoro wakimsililiza mgeni
rasmi wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya
wachunaji wa ngozi wa machinjio ya Manispaa ya Morogoro wakiwa kwenye picha ya
pamoja na mgeni rasmi baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo mjini Morogoro.
Washiriki wa mafunzo ya
wachunaji wa ngozi wa machinjio ya Manispaa ya Morogoro wakiwa kwenye picha ya
pamoja na mgeni rasmi.
Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Felix Nandonde (kushoto) akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo.
Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Felix Nandonde akifafanua
jambo kwa waandishi wa habari kuhusu mpango mkakati wa Wizara hiyo kuhusu mafunzo kwa wachunaji wa
ngozi wa machinjio ya ngozi nchini.
No comments: