LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mbunge asaka zaidi ya Shilingi Milioni 400 kutatua kero ya maji jimboni kwake

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM) akizungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mtavira, Kata ya Makilawa, Wilaya Ikungi mkoani Singida.
Kikundi cha ngoma kikitoa burudani kwenye mkutano huo.
Burudani ikiwa imenoga kwenye mkutano huo.
Taswira kwenye mkutano huo.
Wananchi wakifuatilia mkutano huo.
Na DottoMwaibale, Singida
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Wilaya Ikungi mkoani Singida, Elibariki Kingu ameeleza kusaka kiasi cha shilingi milioni 480 kwa ajili ya kuchimba visima virefu vya maji katika vitongoji 12 vilivyopo Kata ya Makilawa wilayani humo.

Kingu aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wenye lengo la kuhamasisha maendeleo pamoja na kupokea changamoto za wananchi.

"Hapa Mtavira mnapata maji mengi kupitia mradi wa Tanjet, sasa hivi naelekeza nguvu zangu kupeleka maji katika vitongoji 12 vya Kata hii ambapo nitachimba visima 12 vyenye thamani ya shilingi milioni 480 pamoja na ujenzi wa sekondari" alisema Kingu.

Kingu alivitaja vitongoji hivyo kuwa ni Magohana A, Magohana B, Itulu, Kazizi, Munyu, Mpembu, Majengo, Mteva Kati, Songambele, Kasela, Kinyalambe na Darajani.

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa Shule ya Sekondari, Kingu alisema kwa kuanza atachangia mifuko ya saruji 150 huku madiwani wakiahidi kutoa mifuko 10. Alisema miradi yote hiyo inafanyika kwa msaada mkubwa wa Rais Dkt. John Magufuli baada ya kuziba mianya ya fedha za Serikali ambazo zilizokuwa zikitumika vibaya na mafisadi.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Rais Dkt.John Magufuli miradi mingi ya maendeleo imefanyika na mingine inaendelea kujengwa. Alisema katika jimbo la Singida Magharibi baadhi ya miradi mikubwa iliyofanyika ni ya maji na ujenzi wa vituo vya afya vya kisasa katika Kata za Sepuka na Ihanja.

Kingu aliwahimiza wananchi kutunza miundombinu ya miradi hiyo baada ya kukamilika na kueleza kuwa itakuwa haina maana miradi iliyogharamiwa na Serikali kwa fedha nyingi ikaachwa iharibike.

Naye Diwani wa Kata ya Makilawa, Hassan Mtakii alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na mbunge huyo za kuwaletea maendeleo wananchi wa Kata hiyo na nchi nzima kwa ujumla.

No comments:

Powered by Blogger.