Zaidi ya wanafunzi 300 wapachikwa mimba wilayani Magu
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Wanafunzi wa
kike 301 katika Wilaya Magu mkoani Mwanza wameelezwa kukatisha masomo katika
kipindi cha mwaka 2016/19, baada ya kupata ujauzito huku zaidi ya asilimia 90
wakitoka katika Shule za Sekondari.
Mkuu wa Polisi
Dawati la Jinsia na Watoto wilayani Magu, Amani Migoha alitoa takwimu hizo
Agosti 13, 2019, kwenye kikao cha utoaji elimu ya kupambana na ukatili wa
kijinsia katika jamii kwa madiwani, watendaji na viongozi mbalimbali wa
Halmashauri ya Wilaya Magu.
Migoha alisema
mwaka 2016 kesi za mimba/ ndoa za utotoni zilizoripotiwa polisi zilikuwa 71,
2017 kesi 67, 2018 kesi 106 na mwaka huu tayari kesi 57 zimeripotiwa na kwamba changamoto
ya utoaji ushahidi imekuwa ikikwamisha kesi hizo kupata mafanikio mahakamani.
Akifungua
kikao hicho, Mkuu wa Wilaya Magu, Dkt. Philemon Sengati aliwataka viongozi wilayani
humo kila mmoja kutimiza wajibu wake ipasavyo ikiwemo kutoa elimu hadi ngazi ya
jamii ili kuhakikisha matukio ya aina hiyo yanatokomezwa.
Baadhi ya
washiriki wa kikao hicho walitoa baadhi ya sababu walizoshauri zitafutiwe
ufumbuzi ili kupambana na hali hiyo kuwa ni pamoja na ujenzo wa mabweni
hususani kwa wanafunzi wa kike ili kuwaepusha na vishawishi wanapotembea umbali
mrefu kwenda shule na kukemea tabia ya baadhi ya wazazi na walezi kuwashawishi
watoto wao kuolewa ili wapate mahari.
Kikao hicho
ni mwanzo wa utayari kwa viongozi na watendaji mbalimbali wilayani Magu katika
kuelekea kwenye utekelezaji kwa vitendo kampeni/ mpango mkakati wa kitaifa wa
kupambana na aina zote za ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto (MTAKUWWA)
kwa kushirikiana na shirika la kutetea haki za wanawake na wasichana (KIVULINI)
wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya Magu, Dkt. Philemon Sengati akizungumza kwenye kikao hicho.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Magu, Hilal Elisha akichangia mada kwenye kikao hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akisisitiza jambo kwenye kikao hicho.
Baadhi ya viongozi na watendaji waliohudhuria kikao hicho.
Viongozi na wadau mbalimbali waliohudhuria kikao hicho.
Wadau wakifuatilia kikao hicho.
Tazama BMG Online TV hapa chini
SOMA>>> UWT wakutana wilayani Magu
No comments: