LIVE STREAM ADS

Header Ads

Watanzania wahimizwa kushiriki mbio za kimataifa za Rock City Marathon 2019

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
 Mkuu wa Wilaya Nyamagana mkoani Mwanza, Dkt. Philis Nyimbi (kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mbio za kimataifa za Rock City Marathon 2019 zinazoandaliwa na kampuni ya Capital Plus International. Dkt. Nyimbi alifanya uzinduzi huo ulifanyika Septemba 19, 2019 katika viunga vya Rock City Mall kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella.
Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Dkt. Philis Nyimbi (katikati) akijiandikisha kushiriki mbio za Rock City Marathon 2019. Wanaoshuhudia ni Mratibu wa mbio hizo, Magdalena Laizer (kushoto) pamoja na Katibu wa Chama cha Riadha Mkoa Mwanza, Peter Mugaya (kulia)
Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Dkt. Philis Nyimbi (katikati) akionesha medali baada ya kujiandikisha kushiriki mbio hizo. Wanaoshuhudia ni Mratibu wa mbio hizo, Magdalena Laizer (kushoto) pamoja na Msimamizi wa Rock City Marathon, John Bayo (kulia).

Judith Ferdinand, BMG
Mkuu wa Wilaya Nyamagana mkoani Mwanza, Dkt. Philis Nyimbi amezindua rasmi mashindano ya kimataifa ya mbio za riadha ya Rock City (Rock City Marathon 2019) msimu wa 10 yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 20, 2019 jijini Mwanza.

Akizundua mbio hizo Septemba 19, 2019 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongela katika viunga vya Rock City Mall, Dkt. Nyimbi aliwashukuru waandaji wake kwa kazi kubwa wanayoifanya huku akiwahimiza wakazi wa Mkoa Mwanza kujiandikisha kwa wingi ili kushiriki mbio hizo kwani mbali na kuwafanya washiriki kuwa na utambuzi na kutangaza utalii pia michezo ni afya.

"Nawaomba wananchi wa Mkoa wetu mjitokeze kwa wingi kujiandisha ili muweze kushiriki kwa wingi, hata RC wetu Mongela amenihakikishia atashiriki kikamilifu katika mbio hizi hivyo na mimi nitashiriki kikamilifu" alisisitiza Dkt. Nyimbi.

Naye Mwenyekiti wa Rock City Marathon, Magnalena Laizer alisema lengo la mashindano hayo ni kutangaza utalii ikizingatiwa kwamba ukanda wa Ziwa Victoria una vivutio vingi ambavyo lazima vitangazwe kimataifa pamoja na kuhamasisha jamii kupinga mauaji kwa watu wenye ualbino kutokana na imani potofu za kishirikina.

"Mbio hizi zinaweza kuwa chachu ya kufanikisha suala hili la kutangaza utalii kwani mashindano haya yanahusisha mbio za km 42 zinazowavutia zaidi washiriki kutoka nje ya nchi ambapo wadhamini wetu kwa msimu huu wa 10 ni Rock City Mall, Pepsi, Mwanza Water Pure Drinking, SAUT, Metro FM, TANAPA, Bodi ya Utalii Tanzania, Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro, NMR, CF Hospital, Pegeon Hotel, The Cask Bar, Wakala wa Misitu Tanzania na wengine wengi"alibainisha Laizer.

Kwa upande wake Mratibu wa mbio hizo, John Bayo alisema kwa mwaka huu zitaanzia na kumalizikia katika viwanja vya Rock City Mall ambapo zitashirikisha mbio za km 42, km 21 kwa wanawake na wanaume km tano ngazi ya "corporate", km 3 kwa ajili ya watu wenye ualbino na wazee zaidi ya miaka 55 pamoja na km 2.5 kwa watoto kuanzia miaka 7-10 ambapo mbio hizo zinaandaliwa na kampuni ya Capital Plus International.

No comments:

Powered by Blogger.