LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wananchi washauriwa kutumia fursa hii kusajili laini zao za simu kwa alama za vidole

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Na Judith Ferdinand, BMG
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na makampuni ya simu, imeanza kampeni ya kusajili laini za simu kwa alama za vidole kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa ijulikanayo kama "mimi nimesajili laini wewe unangoja nini".

Hatua hiyo inakuja baada ya zoezi la usajili wa laini za simu kwa alama za vidole kusuasua katika maeneo mbalimbali hususani visiwani ambapo lengo ni kufikia watu wengi na kuhakikisha hadi ifikapo mwisho wa zoezi hilo Disemba 31, 2019 wananchi kwa asilimia kubwa wawe wamekamilisha usajili huo.

Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 27, 2019 jijini Mwanza, Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Francis Mihayo alisema wananchi wengi bado hawajasajili laini zao za simu kwa mfumo wa alama za vidole kutokana na makampuni ya simu kushindwa kufikia maeneo ya visiwani ikiwemo kisiwa cha Izumacheli, Bugoro, Lugata, Luhuza, Maisome, Nyakasasa, Kome, Ukerewe, Lulegeya na Butwa.

"Baada ya kubaini hali hiyo, TCRA Kanda ya Ziwa kwa kushirikiana na kampuni zinazotoa huduma ya simu pamoja na NIDA tumekuja na kampeni ijulikanayo kuwa "mimi nimesajili namba yangu ya simu, wewe unangoja nini" ili kuhakikisha wananchi wote wanasajili laini zao za simu kabla ya tarehe ya mwisho ya zoezi hilo ambapo tutazunguka katika mikoa yote sita ya Kanda ya Ziwa ikiwemo ya visiwani na itakuwa inatumia siku saba katika eneo moja hivyo tunaanza Septemba 30, 2019 hadi Oktoba 06, 2019 katika uwanja wa Rock City Mall jijini Mwanza na baadaye maeneo mengine" alisema Mhandisi Mihayo.

Aliwahimiza wananchi kutumia fursa hiyo kusajili laini zao za simu na kwa wale ambao hawakujiandikisha NIDA kwa ajili ya kupata kitambulisho cha taifa, wafike maeneo na kujiandikisha ili waweze kupata namba za kitambulisho zinazotumika kukamilisha na kusajili laini zao kwa alama ya vidole.

"Watoa huduma wa Makampuni yote ya simu watakuwepo, NIDA pia watakuwepo na sisi TCRA tutakuwepo ili kuhakikisha huduma inapatikana kwa urahisi na kumfikia kila mwananchi atakayefika maeneo hayo kwa ajili ya kusajili laini yake kwa alama za vidole, nawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi na kuitumia fursa hiyo ipasavyo" alisema Mhandisi Mihayo.

Nao watoa hudumza ya simu kanda ya Ziwa ambao ni pamoja na Yusuph Salum kutoka Airtel, Jalili Senkopwa kutoka TTCL na Beatrice Kinabo kutoka Tigo waliipogeza TCRA kwa kuanzisha kampeni hiyo huku wakiahidi kutoa huduma ya usajili kwa alama za vidole katika maeneo yote hadi visiwani.

Naye Afisa wa NIDA Mkoa Mwanza, Raphael Manase alisema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa kwa asilimia 100 kwa kushirikiana na makampuni yanayotoa huduma za simu pamoja na TCRA kwa kuwapatia wananchi huduma bora.

Aidha alikemea vikali tabia ya baadhi ya Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Vitongoji kuwatoza pesa wananchi wanaohitaji fomu za NIDA ili waweze kujaza na kupata vitambulisho kwa kusema kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha Sheria kwani fomu hizo haziuzwi na hutolewa bure.

"Sisi NIDA huwa tunapeleka fomu za kutosha katika ofisi za Wenyeviti wa Mitaa au Vitongoji lakini kumekuwa na malalamiko mengi ya baadhi ya viongozi kuwaomba kiasi cha pesa wananchi wanaohitaji fomu hizo kwa madai kuwa fomu hazipo na hiyo pesa ni kwa ajili ya kutoa "photo copy (nakala ya fomu), hiyo haikubaliki na hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa yeyote atakayebainika kufanya hivyo" alisema Manase.
Tazama BMG Online TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.