LIVE STREAM ADS

Header Ads

Biteko aagiza mabadiliko kwa wafanyabiashara wa madini

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Waziri wa Madini, Doto Biteko akifungua mkutano wa wafanyabiashara wa Madini uliofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza jambo na baadhi ya wafanyabiashara wa Madini. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula.
Baadhi ya wafanyabiashara wa Madini wakifuatilia mkutano huo.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakifuatilia semina iliyotolewa na Wizara ya Madini kuhusu Serikali kuamua Chuo Cha Madini Dodoma kilelewe na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Asteria Muhozya na Tito Mselem, Dodoma
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameiagiza Tume ya Madini kuandaa haraka utaratibu utakaowawezesha wafanyabiashara wa madini nchini kufanya shughuli zao katika ngazi ya Kanda tofauti na ilivyo sasa ambapo taratibu zinawataka kufanya shughuli hizo katika mikoa zinapotolewa leseni zao.

Biteko aliyasema hayo Septemba 7, 2019 wakati wa mkutano wa wafanyabiashara wa madini na wizara hiyo uliofanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi, wataalam pamoja na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.

Aidha Waziri Biteko alieleza kuwa endapo wadau hao watafanya shughuli zao kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizowekwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kutanua wigo kuwawezesha kufanya biashara ya madini katika maeneo mengi zaidi.

Waziri Biteko alisisitiza kuhusu ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ya kutaka rasilimali madini kulinufaisha Taifa na watanzania na kueleza kuwa ndoto hiyo ndiyo iliyopelekea kufanyika kwa mageuzi mkubwa katika Sekta ya Madini.

Alikiri kuwa kabla ya mabadiliko hakukuwa na mfumo rasmi uliowaonesha wachimbaji kujua sehemu sahihi ya kuuzia madini yao vivyo hivyo kwa wanunuzi wa madini suala ambalo lilipelekea kuwepo vitendo vya utoroshaji madini jambo ambalo lilionekana ni la kawaida.

Waziri Biteko aliwataka wafanyabishara hao kuyatumia masoko yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali nchini na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kudhibiti vitendo vya utoroshaji madini na kwamba waliobainika kufanya vitendo hivyo wataanza kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Akijibu hoja zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabishara wa Madini ya Vito (TAMIDA), Sam Mollel kuhusu changamoto ya ucheleweshaji wa vibali vya kusafirisha madini nje ya nchi, Waziri Biteko aliwataka kuwa na subira wakati Serikali ikishughulikia suala hilo.

Aidha akijibu changamoto ya masonara kusimamiwa na wizara nyingine, Waziri Biteko aliwataka wafayabiashara hao kuwasilisha maoni kuhusu suala hilo kama ilivyofanyika katika kuandaa Kanuni za Masoko na kuongeza kwamba lengo la Wizara ya Madini ni kutatua matatizo na changamoto mbalimbali.

Naye Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alisisitiza kuhusu suala la kulipa kodi kama inavyowapasa na kuwataka kuyafahamu mabadiliko yaliyofanywa katika sekta na kuwa sehemu ya mabadiliko hayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula aliipongeza wizara kwa kazi ya kuwalea wadau wa madini na kueleza kwamba miaka ya nyuma mambo mengi kwenye sekta hiyo hayakuwa yakienda vizuri. 

Aidha aliwapongeza wafanyabiashara wa madini na kueleza kuwa hivi sasa wameanza kubadilika huku tabia ya kufanya biashara ya madini kiholela ikianza kutoweka. "Sisi Kamati tunapoona mambo yanakwenda vizuri mnaturahisishia kazi yetu" alisisitiza Kitandula.

Mkutano huo ni sehemu ya jitihada za Wizara ya Madini kuendelea kutoa elimu kwa wadau wa madini ikiwemo kusikiliza na kutatua changamoto kwenye sekta jiyo ili kuwezesha biashara ya madini kufanyika katika mazingira mazuri yanayoleta tija kwa pande zote. 

Sambamba na mkutano huo pia ilifanyika semina kwa wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini ikitoa fursa kwa Serikali kueleza nia yake ya kukifanya Chuo Cha Madini Dodoma kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 

Akifungua semina hiyo, Kitandula alitaka mchakato wa wa kukilea Chuo hicho kutochukua muda mrefu na alikitaka kijisimamie chenyewe ndani ya muda mfupi baada ya kulelewa na kutoa elimu bora huku akitaka kozi ya mafundi mchundo kuwekewa msingi mzuri.

Pamoja na hayo, aliitaka Wizara ya Madini kukiongezea nguvu Kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC) ikiwemo bajeti ya kutosha ili kukiwezesha kuboresha miundombinu yake.

Tazama BMG Online TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.