LIVE STREAM ADS

Header Ads

Asasi za Kiraia zaomba Serikali kutoa unafuu wa kodi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa akizungumza na wanahabari baada ya kufunguliwa kwa mkutano wa tano wa Wakurugenzi wa Asasi za Kiraia (AZAKI) jijini Mwanza, Oktoba 13, 2019. 

Judith Ferdinand, BMG
Jukwaa la Wakurugenzi wa Asasi za Kiraia (AZAKI) nchini Tanzania limeiomba Serikali kutoa unafuu wa kodi kwa asasi hizo ili ziweze kufanya shughuli zake vyema na hivyo kutoa mchango katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Mratibu Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alitoa ombi hilo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa tano wa Wakurugenzi wa Asasi za Kiraia (AZAKI) unaofanyika kwa siku mbili jijini Mwanza kuanzia Oktoba 13, 2019.

Olengurumwa alisema kati ya changamoto nyingi za kisheria zinazoathiri utendaji wa AZAKI ni pamoja na masuala ya msamaha wa kodi hasa katika mazingira ya jinsi gani mashirika yanapata hifadhi ya hisani kwa ajili ya unufaikaji wa msamaha huo licha ya kufanya kazi nzuri ambayo ni ya kujitolea katika nyanja mbalimbali ikiwemo utetezi wa haki za binadamu, uchechemuzi katika maeneo kadhaa, usambazaji wa huduma za kijamii hivyo inapaswa mchango huo utambulike kwa kusamehewa kodi hususani kodi inayotokana na faida.

"Sekta ya Asasi za Kiraia nchini ni muhimu kwani inachangia maendeleo mbalimbali ya jamii ikiwemo kuchangia fedha za kigeni, elimu kwa kujenga shule, afya kwa kujenga zahanati, kilimo, kutoa elimu ya uraia na pia ajira takribani laki tano ambapo fedha wanazozipata zinatokana na wadau kutoka nje ya nchi ambazo ni za msaada hivyo tunaomba Serikali kutoa unafuu wa kodi kwa baadhi ya maeneo ikiwemo kodi ya faida, tunafanya kazi ya kujitolea siyo kama mashirika mengine yanayotafuta faida" alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo, Kamishina wa Sera za Bajeti kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Shogholo Msangi alisema,kwa mujibu wa sheria ni wazi kwamba pamoja na kuwepo kwa mazingira mbalimbali ya kisheria ambayo asasi za kiraia zinaweza kusamehewa kodi AZAKI kwa ujumla zinawajibu wa kufuata matakwa ya sheria hizo ikiwemo kulipa kodi.

"Kupitia mkutano huu napenda kutoa wito kwenu wanaa AZAKI wote kuzingatia sheria hizi kwa vitendo ili kwa pamoja tuendelee kulijenga Taifa letu, ninatambua kuwa katika sheria zetu na utekelezaji wake katika taasisi husika za Serikali, hazikosi changamoto mbalimbali zinazoweza kupunguza ufanisi katika kazi zenu na zoezi zima la ulipaji wa kodi, hivyo sehemu hii ni muhimu mnayoweza kuitumia kujadili changamoto zote za kisheria na kisera ili ziweze kutatuliwa na pale ambapo Serikali itahitaji kuboresha mazingira ya kisheria na kisera msisite kuyaleta mapendekezo yenu kwetu na sisi tutayafanyia kazi" alisema Msangi

Aidha Msangi alisema sekta ya AZAKI imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo lakini bado sekta hiyo haijaweza kurekodi vizuri mchango wake katika maendeleo ya nchi kutokana na kuongozwa na sheria tofauti tofauti huku usajili na utendaji kazi wake ukiwa chini ya taasisi tofauti za kiserikali hivyo ni wakati mwafaka kwa asasi hizo kukaa pamoja na Serikali ili kufanya tathimini ya kina na kuona ni kwa namna gani zitaweza kuweka utaratibu mzuri wa kupima mchango huo kwa Taifa.

Naye Mkurugenzi wa Uratibu wa AZAKI kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Andrew Komba alizitaka asasi za kiraia kurasimisha shughuli zake nchini ili ziweze kutambulika kisheria na katika mipango ya Serikali.

Mkutano huo wa Wakurugenzi wa AZAKI Tanzania ulikuwa na dhima kuhusu "kodi zinazohusiana na AZAKI na mchango wake kwa maendeleo ya Taifa".

No comments:

Powered by Blogger.