LIVE STREAM ADS

Header Ads

Watumishi wa afya mkoani Mbeya 'kitanzini"

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Ziara ya Naibu Katibu Mkuu OR- TAMISEMI anayeshughulikia sekta ya afya, Dkt. Dorothy Gwajima (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila (kushoto) baada ya kuwasili ofisini kwake kabla ya kuanza ziara ya kikazi mkoani humo.
Ziara ya Naibu Katibu Mkuu OR- TAMISEMI anayeshughulikia sekta ya afya, Dkt. Dorothy Gwajima akizungumzia ziara yake baada ya kufika katika Halmashauri ya Busokelo ambapo alikagua ujenzi wa Kituo cha Afya cha Isange kilichopatiwa Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa majengo manane kikitarajiwa kuanza kutoa huduma kwa wananchi Januari 2020.
Ziara ya Naibu Katibu Mkuu OR- TAMISEMI anayeshughulikia sekta ya afya, Dkt. Dorothy Gwajima akizungumzia ujenzi wa jengo la Hospitali ya Wilaya Busokelo mkoani Mbeya ambapo Serikali ilitoa shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi huo.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Busokelo mkoani Mbeya, Ramadhani Hussein akitoa ufafanuzi kwa Ziara ya Naibu Katibu Mkuu OR- TAMISEMI anayeshughulikia sekta ya afya, Dkt. Dorothy Gwajima alipofanya ziara hiyo katika Hospitali Teule ya Itete.
Mwonekano wa moja ya majengo ya Hospitali mpya ya Halmashauri ya Busokelo mkoani Mbeya.

Na Atley Kuni, Mbeya
Serikali imetoa wiki mbili kwa timu ya Afya ya Halmashauri ya Busokelo mkoani Mbeya kutoa maelezo ya kina kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, kama ina uhalali wa kuendelea na majukumu yao yakusimamia Afya kwenye Halmashauri kutokana na uzembe mkubwa uliobainiwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Daktari Dorothy Gwajima wakati wa ziara yake ya kikazi.

Dkt. Gwajima alifikia azma hiyo baada ya kutembelea Hospitali ya Halmashauri (Itete) na kusomewa taarifa ya afya ambayo haijibu hoja za msingi ikiwemo usimamizi wa fedha, ushirikishwaji wa wajumbe wa timu ya usimamizi katika taarifa za mapato na matumizi ya fedha na utekelezaji wa mipango kwa ujumla.

Aidha Dkt. Gwajima alibaini hakuna taarifa za usimamizi wa vituo wala muhtasari wa vikao na michache iliyopo haijawahi kuthibitishwa wala haija fuata kalenda ya vikao kwa mujibu wa taratibu

"Hivi inakuwaje Mganga Mkuu wa Halmashauri huna muda na majukumu yako huelewi mambo ya msingi kifupi huna habari" alihoji Dkt Gwajima na kuongeza;

"unao wajumbe wa timu ya afya idadi imekamilika, unao makatibu wa afya wawili, mnavyo vituo 22 tu vya kutolea huduma na vyote vinafikika, halafu hamjui chochote kinachoendelea, kwani mkiingia kazini huwa mnafanya nini hasa? Nako huko stoo ya dawa kumbukumbu haziko vizuri hii inakuwaje na kila siku tunaelimishana?" alizidi kuhoji huku akionesha kukerwa na mwenendo wa timu hiyo.

Kufuatia mambo kwenda ndivyo sivyo Naibu Katibu Mkuu alimuagiza Mkurugenzi kwamba ndani wiki mbili Mganga Mkuu Wilaya awe ametoa taarifa ya kina kwake lakini pia taarifa hiyo imfikie Katibu Tawala wa Mkoa pamoja na Katibu Mkuu TAMISEMI, ikitoa sababu za msingi kwa nini wasichulikuwe hatua za kinidhamu kwa kushindwa kutimiza wajibu wao.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Busokelo Eston Ngilingwa, amekiri ziara hiyo ya Naibu Katibu Mkuu kumfumbua Macho na kuanzia sasa atatumia mbinu na mikakati hiyo na kufanya suala la dawa kuwa ajenda mtambuka na ya kudumu kwa viongozi wote wa Halmashauri hiyo wanapokutana lakini pia Mkoa.

"Ndugu Naibu Katibu Mkuu kwa kweli mimi umenipa somo jipya ambalo hata kuongea nashindwa niongee nini maana kila ulichokiona hapa hakuna mtu ambaye anaweza kusema amesingiziwa, hivyo naomba kuahidi kufanyia kazi maelekezo yako na nitatoa taarifa mimi mwenyewe" alisema Ngilingwa.

Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo Dkt. Ramadhani Hussein, mbela ya Naibu Katibu Mkuu, alikiri kushindwa kusimamia eneo lake la kazi huku akiomba msamaha kwa kushindwa kufanya hivyo na kuahidi kubadili katika utendaji wake.

Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, anayeshughulia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima, amekuwa na muendelezo wa Ziara zake kwenye Mikoa mbalimbali nchini kujionea uendeshaji wa shughuli za Afya kwa Ngazi ya Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya pamoja na Zahanati, ambapo kote anakopita amekuwa akisisitiza watumishi wa kubadilika kifikra na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwani katika awamu ya sasa ya Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye ameamua Taifa lifikie uchumi wa kati ifikapo 2025, lazima suala la Afya liwe kipaumbele namba moja kwa wananchi.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.